KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA PROGRAMU YA BBT CHINANGALI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi imefanya ziara tarehe 19 Aprili 2026 mkoani Dodoma, katika shamba la pamoja la Chinangali, kujionea utekelezaji wa programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), pamoja na kutathmini mafanikio na changamoto zilizopo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb) amepongeza hatua kubwa iliyofikiwa katika Programu hiyo. Ameeleza uwekezaji uliofanyika katika miundombinu ya barabara pamoja na ujenzi wa mabwawa makubwa ya umwagiliaji umeleta mwanga mpya wa maendeleo kwa vijana na wanawake wanaoshiriki katika Programu hiyo.
Aidha, amewahimiza vijana kuendelea kujituma na kuongeza ubunifu katika matumizi ya miundombinu iliyopo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija, hususani katika kilimo cha mbogamboga. Ameongeza kuwa Kamati inajivunia mafanikio hayo na itayatumia kama ushahidi chanya wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2026/2027.
Ziara hiyo pia imehudhuriwa na Mhe. David Silinde (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo,; Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo; Mha. Athumani Kilundumya, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo,; Wataalam wa Wizara na Wanufaika wa Programu ya BBT Chinangali.
Naye Naibu Waziri Silinde ameeleza kuwa programu ya BBT ni endelevu na inalenga kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi kupitia uwekezaji katika sekta ya kilimo. Aidha, Katibu Mkuu Mweli amewahimiza vijana kuzingatia nidhamu ya kifedha kwa kuweka akiba kwa ajili ya maandalizi ya mashamba yao, akibainisha kuwa tayari wamekabidhiwa jumla ya hekari 1,770 katika eneo la Chinangali. Pia ameahidi Wizara itaendelea kuwatafutia masoko ya uhakika kwa mazao yao.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mweli ameeleza kuwa kupitia BBT Halmashauri, Wizara ina mpango wa kuanzisha mashamba 20 mapya katika halmashauri 20 nchini, kila moja likiwa na hekari 500, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwafikia wakulima wengi zaidi na kukuza sekta ya kilimo nchini.