KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA UJENZI WA MAABARA YA MBEGU TOSCI
Tanzania ya kesho inatengenezwa na mapinduzi ya kilimo kupitia sayansi na tafiti za kuwezesha upatikanaji wa mbolea na mbegu bora, viuatilifu na afya ya udongo inayofaa kwa kilimo.
Yamesemwa hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Deodatus Mwanyika (Mb), akiwemo Makamu Mwenyekiti Mhe.Mariam Ditopile (Mb) na wajumbe wake walipotembelea mradi wa ukarabati na ujenzi wa Maabara ya mbegu ya Taifa ya Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), tarehe 15 Machi 2026, Mkoani Morogoro.
Kamati hiyo pia imeipongeza Wizara ya Kilimo na Taasisi yake ya TOSCI kwa kazi nzuri ya ujenzi wa maabara na kusema ni moja ya mradi mzuri wa mfano hususan na hatua ya asilimia 86 ujenzi ulipofikia. “Ongezeni nguvu kwenye kushughulika na mbegu feki na toeni elimu ya kutosha kwa wakulima kuhusu mbegu zilizothibitishwa,” amesisitiza Mwenyekiti Mhe. Mwanyika.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) ameishukuru Kamati kwa kukagua maabara ya TOSCI ambayo ni ya kisasa yenye kugharimu Shilingi Bilioni 1.98 kwa ajili ya kufanya tafiti na kuthibitisha mbegu bora.
“Uthibiti wa mbegu unaendana sambamba na jukumu la TOSCI kudhibiti uuzaji wa mbegu zisizothibitishwa (feki) ili kuepusha madhara yoyote kwa jamii ili mlaji awe na uhakika wa ubora kwa kilichozalishwa,” Amesema Waziri Chongolo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Bw. Nyasebwa Chimagu amesema kuwa Taasisi yake inahamasisha na kuwezesha uwekezaji ili jukumu la uthibitishwaji wa mbegu kuimarika.
Akitoa salamu za kupokea ugeni huo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kuwa Mkoa huo ni mfano wa mapinduzi ya kilimo na kuwa una ardhi yenye rutuba ya kilimo cha mazao yenye msukumo wa kibiashara akitolea mfano wa karafuu, kokoa, parachichi, kahawa, michikichi, miwa, mpunga na mengine mengi.