KAMPUNI YA TOYO YA JAPAN KUJENGA KIWANDA CHA MBOLEA NCHINI
Kampuni ya Toyo Engineering Corporation (TOYO) ya nchini Japan imeonesha nia ya kuwekeza kwenye ujenzi wa kiwanda cha mbolea nchini kwa kutumia gesi asilia na makaa ya mawe katika kuzalisha mbolea mbalimbali ikiwemo ammonia pamoja na Urea.
Hayo yamesemwa wakati wa mkutano kati ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya na Mkurugenzi wa Idara ya Biashara za Kimataifa, Bw. Taisuke Nonaka aliyeambatana na Meneja Mauzo Mwandamizi kutoka Idara ya Biashara za Kimataifa.
Kampuni hiyo inajishughulisha na masuala ya uhandisi, manunuzi, biashara ya ujenzi wa nishati pamoja na miradi ya viwanda Duniani.
Mha. Kilundumya amewaambia wawekezaji kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji katika tasnia ya mbolea ili kuhakikisha kuna utoshelevu wa mbolea nchini na kuongeza kasi ya matumizi ya mbolea kwa wakulima. Amewasihi wawekezaji hao kufanya tafiti za kina kuhusu uwekezaji huo ili unufaishe mahitaji ya wakulima nchini na kuleta tija katika uzalishai wa mazao.