Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

KATIBU MKUU MWELI AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI WA KAMPUNI YA PERRY KUHUSU KUIMARISHA TEKNOLOJIA YA HIFADHI MAZAO

Imewekwa: 15 Apr, 2026
KATIBU MKUU MWELI AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI WA KAMPUNI YA PERRY KUHUSU KUIMARISHA TEKNOLOJIA YA HIFADHI MAZAO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amekutana kwa mazungumzo na Bw. David Perry, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya PERRY Engineering Excellence kutoka nchini Uingereza, inayojishughulisha na uzalishaji wa vifaa vya utunzaji wa mazao baada ya kuvunwa, ikiwemo mifumo ya uchakataji, ukaushaji na uhifadhi.

Majadiliano hayo yamefanyika tarehe 13 Aprili 2026, jijini Dodoma yakihusisha tathmini ya hali ya sasa nchini katika utunzaji wa mazao baada ya kuvunwa na changamoto mbalimbali zinazoathiri ufanisi wa Sekta ya Kilimo.  Pia wamejadili kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa ili kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza thamani katika mnyororo wa uzalishaji.

Akichangia katika majadiliano hayo, Dkt. Andrew Komba, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), ameainisha uzoefu unaotumika nchini katika baadhi ya miundombinu iliyojengwa kwa kutumia teknolojia inayotoka nchini Poland.  Ameeleza kuwa uzoefu huo unaonesha umuhimu wa uwekezaji katika teknolojia za kisasa za uhifadhi wa mazao.

Aidha, Dkt. Komba ameialika Kampuni ya PERRY Engineering Excellence kuangalia fursa ya kuwekeza nchini katika kuendeleza na kuboresha miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya nafaka baada ya kuvunwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya kimataifa, hatua itakayochangia kuongeza ufanisi na kupunguza hasara kwa wakulima.

Katika kuhitimisha mazungumzo hayo, Katibu Mkuu Mweli ameielekeza NFRA kukutana na wataalam wa Kampuni ya PERRY Engineering Excellence kwa lengo la kuandaa andiko dhana (Concept Note) litakalowezesha kuanzishwa kwa mradi wa pamoja unaotarajiwa kusaidia kutatua changamoto za uhifadhi wa mazao baada ya kuvunwa na kuongeza uwezo wa hifadhi hadi kufikia tani milioni 3 ifikapo mwaka 2030, hivyo kuimarisha usalama wa chakula nchini.