MAAFISA UGANI WAHIMIZWA KUTOA HUDUMA BORA KWA WAKULIMA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amewataka Maafisa Ugani kuendelea kutoa huduma na ushauri bora kwa wakulima ili kuwa na matokeo chanya.
Katibu Mkuu Mweli amezindua Mafunzo ya Maafisa Ugani tarehe 17 Aprili 2025 katika Chuo cha Kilimo cha MATI Mlingano, Wilaya ya Muheza, Mkoani Tanga ambapo pia amekabidhi nyumba wilayani Pangani.
Mafunzo hayo yamehusisha Maafisa Ugani kutoka Lushoto, Bagamoyo, Ubungo, Kigamboni kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuwafikia wakulima zaidi ya milioni 13 kwa kutumia mbinu shirikishi kama mifumo ya kidijitali na mashamba darasa.
“Serikali imetoa vifaa muhimu kama pikipiki, vishikwambi na vifaa vya kupimia afya ya udongo kwa Maafisa Ugani, ili kuongeza ufanisi katika huduma zinazotolewa kwa wakulima. Kimsingi, kila Afisa Ugani anapaswa kuamka kila siku akiwa na uelewa wa wakulima wake wako wapi na wanajihusisha na kilimo cha aina gani, ili kuwahudumia ipasavyo,” amesema Katibu Mkuu Mweli.
Ameeleza zaidi kuwa Wizara ya Kilimo imeelekeza Vituo vya Mafunzo kama MATI Mlingano vitaendelea kutoa mafunzo ya kuwaongezea uwezo Maafisa Ugani mara mbili kwa mwaka, ikiwa ni mkakati wa kuwa na wataalamu mahiri wa mazao nchini. “Tunataka kutengeneza Maafisa Ugani waliobobea kwenye mazao husika, tunataka mtu akitoka hapa analijua zao hilo vyema kama mkulima,” amefafanua Katibu Mkuu Mweli.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mweli amezindua rasmi na kukabidhi nyumba ya Afisa Ugani wa Kilimo katika Kijiji cha Masaika, Kata ya Masaika wilayani Pangani mradi uliogharimu Shilingi Milioni 41.5 na kueleza kuwa Serikali chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekusudia kujenga nyumba kwa Maafisa Ugani nchi nzima pamoja na ununuzi wa matrekta ili kurahisisha huduma kwa wananchi wote.