Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MAJALIWA: TANZANIA YAFIKIA UTOSHELEZI WA CHAKULA ASILIMIA 128

Imewekwa: 16 Oct, 2025
MAJALIWA: TANZANIA YAFIKIA UTOSHELEZI WA CHAKULA ASILIMIA 128

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, amesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa mafanikio katika usalama wa chakula Barani Afrika, baada ya kufikia utoshelezi wa chakula kwa asilimia 128 mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 114 mwaka 2021.

Amesema mafanikio hayo yametokana na ongezeko la uzalishaji wa chakula kutoka tani milioni 18 mwaka 2021 hadi kufikia tani milioni 22 mwaka 2025, hatua inayoonesha utekelezaji wa mikakati madhubuti ya Serikali kupitia Wizara ya Kilimo katika kuimarisha Sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Mhe. Majaliwa ametoa mfano wa Mkoa wa Tanga kuwa miongoni mwa maeneo yenye tija kubwa katika uzalishaji wa chakula, ambapo mwaka 2024 ulizalisha tani milioni 1.8 dhidi ya mahitaji halisi ya tani 621,000. Amesema takwimu hizo zinaonesha uwezo mkubwa wa wakulima wa Mkoa huo na mafanikio ya utekelezaji wa sera za Serikali zinazolenga kukuza uzalishaji na usalama wa chakula nchini.

Kwa upande wake, Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania, Bi. Suzan Namondo, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mafanikio makubwa katika Sekta ya Kilimo, akisema kuwa Tanzania imekuwa mfano bora wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan lengo namba mbili linalohusu kutokomeza njaa.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema utekelezaji wa Dira ya Sekta ya Kilimo umeendelea kuchochea ukuaji wa uzalishaji, kuongeza tija na kuimarisha upatikanaji wa chakula nchini. Amesisitiza kuwa Tanzania imeendelea kuuza ziada ya mazao ya chakula katika masoko ya nje, ikiwa ni kielelezo cha ufanisi wa sera na programu za Serikali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian, amesema zaidi ya waoneshaji bidhaa na huduma 578 pamoja na wajasiriamali 70 wameshiriki katika maonesho ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani mwaka huu. Amesema tukio hilo limeonesha hamasa kubwa ya wananchi na wadau wa kilimo, na kuthibitisha nafasi ya Mkoa wa Tanga kama kitovu cha maendeleo ya kilimo na uwekezaji nchini.