Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MAPINDUZI YA SEKTA ZA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KUCHOCHEA UCHUMI WA KATI WA JUU KWA TAIFA

Imewekwa: 13 Feb, 2026
MAPINDUZI YA SEKTA ZA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI KUCHOCHEA UCHUMI WA KATI WA JUU KWA TAIFA

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi iko tayari kushiriki kikamilifu katika Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Shoroba za Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2050 utakaosaidia kuchochea uchumi wa kati wa juu kwa Taifa. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa uhamasishaji wa ukuzaji na uendelezaji wa shoroba za kilimo uliofanyika tarehe 12 Februari 2026, mkoani Singida, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.  Rosemary Senyamule amesema kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kujenga uelewa wa pamoja wa mpango huo kwa wataalam wa Mikoa na Halmashauri kuhusu dhana za kilimo.

“Serikali ya Awamu wa Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika mageuzi ya Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kama kiungo cha kukuza uchumi wa Taifa, kuongeza ajira na kuinua maisha ya Watanzania kwa ujumla,” amesema Mhe. Senyamule. 

Aidha, amesema kuwa mpango huo unalenga kupunguza gharama za uzalishaji na usafirishaji, kuongeza thamani ya mazao, kuongeza kipato cha Wakulima, Wafugaji na Wavuvi pamoja na kuvutia uwekezaji wa Sekta Binafsi kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Senyamule ameongeza kuwa shoroba za kilimo ni nyenzo za kimkakati katika utekelezaji wa mpango huo ili kuunganisha maeneo yenye uzalishaji mkubwa na miundombinu muhimu kama barabara, reli, bandari, masoko na viwanda vya kuchakata mazao.

Naye Mkurugenzi wa Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (Agricultural Transformation Office - ATO), Bi. Elizabeth Missokia amesema kuwa dhana ya shoroba za kilimo ni moja ya mradi ndani ya mpango kabambe wa mageuzi ya sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi  unaounganisha uzalishaji, usindikaji uchakataji usafirishaji na uhifadhi wa masoko ili kuharakisha mageuzi katika sekta hizo.