Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MHE. KASSIM MAJALIWA - USHIRIKA UMELETA FAIDA NCHINI

Imewekwa: 06 Aug, 2025
MHE. KASSIM MAJALIWA - USHIRIKA UMELETA FAIDA NCHINI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema ushirika umeleta faida mbalimbali nchini ikiwemo kuongezeka kwa mauzo ya mazao na kuimarika kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupitia elimu inayotolewa kwa wananchi kuhusu ushirika.

Mhe. Majaliwa amesema tarehe 3 Agosti 2025 katika viwanja vya Maonesho ya Nane Nane vya Nzuguni, mkoani Dodoma akisema Ushirika umekuwa msingi wa kuwaunganisha wakulima, wafugaji na wavuvi katika uzalishaji, uongezaji thamani kupitia viwanda vidogo vidogo na vikubwa pamoja na utafutaji wa masoko ya bidhaa zao.

Amesema kupitia ushirika bei za mazao na masoko zimeimarika yakiwemo masoko kwa njia ya mtandao, akitaja bei ya korosho kupanda kutoka shilingi 1,750 hadi 4,000 kwa kilo; bei ya kahawa kupanda kutoka shilingi 1000 hadi kufikia wastani wa shilingi 3000 hadi 4000 kwa kilogramu moja.

Waziri Mkuu ameeleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuimarisha ushirika ikiwemo uanzishwaji wa Benki ya Ushirika (COOP Bank) ambayo inakua kwa kasi hapa nchini, na kuitaka benki hiyo  kuhakikisha wananchi wanajiunga kupitia vyama vya ushirika ili waweze kuweka akiba na kukopa fedha kwa shughuli za uzalishaji.

Mhe. Majaliwa amehitimisha kwa kutoa onyo kwa viongozi wa vyama vya ushirika wasio waadilifu akisema, Serikali haitovumilia vitendo vyovyote vinavyohatarisha ustawi wa Ushirika na kuwataka viongozi hao kuacha tamaa na badala yake washiriki katika kuongoza vyama hivyo ipasavyo.

Katika tukio lingine, Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pia alipokea tuzo kwa pongezi za mchango wake katika kuimarisha ushirika: pamoja na kutoa tuzo mbalimbali kwa waoneshaji waliofanya vizuri; ikiwa ni pamoja na kutoa tuzo kwa Mhe. Hussein Bashe, Waziri wa Kilimo.