MHE. SILINDE AKUTANA NA UONGOZI WA MKOA WA DODOMA KUJADILI UWEKEZAJI WA ZAO LA TUFAA
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Mkoa wa Dodoma, Kampuni ya Tamu Tamu Tanzania, Wataalam kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Wataalam kutoka Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kujadili uwekezaji wa zao la Tufaa “Apple” katika Mkoa wa Dodoma, tarehe 11 Juni 2025, jijini Dodoma.
Naibu Waziri Silinde amepokea mapendekezo kutoka kwa Bw. Kaspar Mmuya, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuhusu kuiomba Wizara kuwezesha uzalishaji wa miche ya tufaa, na kuwezesha kutoa wataalam kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kushirikiana na Kampuni ya Tamu Tamu kwa kuendelea kufanya utafiti wa zao la Tufaa Mkoani Dodoma.
Ameipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kuwa na mipango ya kuongeza mazao ya kimkakati Mkoani Dodoma ambayo inaenda sambamba na mipango ya Wizara ya Kilimo ya kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo yakiwemo mazao ya bustani ambayo yamekuwa mchango mkubwa wa uingizaji wa fedha za kigeni nchini.
Naibu Waziri Silinde ameeleza kuwa uzalishaji wa zao la tufaa mkoani Dodoma kutapunguza uagizaji wa matufaa kutoka nje ya nchi. Amesema kuwa Wizara itawezesha uzalishaji wa miche ya tufaa na kutoa wataalam kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).