Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MIKOA SABA KUNUFAIKA NA KILIMO CHA UMWAGILIAJI KWA WAKULIMA WADOGO

Imewekwa: 24 Oct, 2025
MIKOA SABA KUNUFAIKA NA KILIMO CHA UMWAGILIAJI KWA WAKULIMA WADOGO

Wakulima wadogo katika mikoa saba nchini watanufaika na mpango wa kilimo cha umwagiliaji unaolenga kuwawezesha kuondokana na utegemezi wa mvua za msimu na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kibiashara.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela vilivyopo Nzuguni jijini Dodoma, tarehe 24 Oktoba 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendeleza kilimo chenye tija kwa wakulima wadogo nchini.

Katibu Mkuu Mweli amebainisha  kuwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango huo itahusisha mikoa saba ya Mara, Mwanza, Simiyu, Kagera, Geita, Ruvuma na Tanga, ambapo jumla ya wilaya 16 na vijiji 93 vitanufaika.

Katika awamu hiyo, wakulima 2,264 watafikiwa na jumla ya hekta 4,000 zitamwagiliwa kupitia mfumo huo wa umwagiliaji.  Baada ya miezi sita, mpango huo utaendelea katika awamu ya pili kwa mikoa mingine nchini.

Katibu Mkuu Mweli ameeleza kuwa wakulima wataunda vikundi vya ushirika ambapo kikundi cha watu 10 kitapatiwa pampu moja, huku kikundi cha watu 30 kikipewa pampu tatu.

Pampu hizo aina ya Jet 35, zenye thamani ya shilingi bilioni 3.5, zina uwezo wa kumwagilia umbali wa mita 500 kutoka chanzo cha maji na ekari moja kwa saa.  Aidha, katika awamu ya kwanza, visima 500 vitachimbwa ili kuwezesha upatikanaji wa maji ya kutosha kwa wakulima.

Katibu Mkuu Mweli ameongeza kuwa  utekelezaji wa mpango huu utasaidia kuongeza tija na uzalishaji, hasa kwa wanawake na vijana wanaojihusisha na kilimo cha mbogamboga, matunda na mazao mengine ya kibiashara.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya umwagiliaji ili kuhakikisha wakulima hawategemei mvua, hivyo kuongeza kipato na usalama wa chakula nchini.