Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MIRADI NA MIKATABA YA WIZARA YA KILIMO KUIMARISHWA UTEKELEZAJI WAKE

Imewekwa: 09 Mar, 2026
MIRADI NA MIKATABA YA WIZARA YA KILIMO KUIMARISHWA UTEKELEZAJI WAKE

Miradi yote inayotekelezwa chini ya Wizara ya Kilimo imeelekezwa kuzingatia kikamilifu sheria, taratibu na kanuni za Serikali ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Ameelekeza hayo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya wakati akifunga rasmi mafunzo ya siku kumi na tano (15) kuhusu Usimamizi wa Miradi na Mikataba yaliyotolewa kwa Wahandisi wa Wizara ya Kilimo na Taasisi zake, tarehe 6 Machi 2026, Viwanja vya Nzuguni, Nanenane jijini Dodoma.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kwa lengo la kuwajengea uwezo wahandisi katika usimamizi bora wa miradi na mikataba kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji, ufanisi na thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Kilundumya amesema Wizara inadhamiria kuwa taasisi imara inayosimamia miradi ya maendeleo kwa weledi, uwazi na kwa kuzingatia misingi ya kitaaluma. Amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kuwajengea uwezo wahandisi na wasimamizi wa miradi kupitia mafunzo ya mara kwa mara ili kuhakikisha miradi ya Serikali inatekelezwa kwa viwango vinavyotarajiwa na kwa muda uliopangwa.

Katika hatua nyingine, Mha. Kilundumya ameipongeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mafunzo hayo, hususan kwa kuleta wataalamu wabobezi waliotoa elimu ya kina kuhusu usimamizi bora wa miradi. Amesema Wizara ya Kilimo itaendelea kushirikiana na ERB katika kuandaa na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa sekta hiyo ili kuimarisha utaalamu katika usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa maslahi ya umma.

Mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli tarehe 16 Februari 2026 na kuhusisha washiriki 96 kutoka Wizara ya Kilimo na Taasisi zake.