Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MIRADI YA UMWAGILIAJI YAKUZWA NA UDHIBITI WA PEMBEJEO FEKI WAIMARISHWA

Imewekwa: 12 Mar, 2026
MIRADI YA UMWAGILIAJI YAKUZWA NA UDHIBITI WA PEMBEJEO FEKI WAIMARISHWA

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imewahakikishia wakulima wa Mkoa wa Rukwa kunufaika na miradi ya umwagiliaji  thaman iya Shilingi Bilioni 51.9 huku ikiwataka wakulima kuwa makini wanaponunua mbegu za ruzuku kwa kuhakikisha zina lebo ya Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).

Amesema Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungamo Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) tarehe 9 Machi 2026, katika Wilaya ya Nkasi, Mkoani Rukwa.

 Mhe. Silinde amesema kuwa katika Wilaya ya Nkasi, miradi ya umwagiliaji inayotekelezwa ina thamani ya shilingi bilioni 21.1 ambayo ni pamoja na mradi wa umwagiliaji wa Katongolo, wenye thamani ya shilingi bilioni 20.98.  Ameeleza kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2023 na kupangwa kukamilika mwezi Juni 2026, umeongezewa muda hadi Desemba 2026 ili kuhakikisha unakamilika kwa ubora unaotakiwa.

Kuhusu ununuzi wa mazao, amesema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) utaendelea kununua mahindi kutoka kwa wakulima kulingana na bajeti iliyopo, kwa lengo la kutekeleza maelekezo ya kuhakikisha kuna soko la uhakika kwa wakulima wa mahindi.

Katika kulinda ubora wa pembejeo za kilimo, Mhe. Silinde amesisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wauzaji wa mbegu feki na mbolea feki.  Wauzaji watakaobainika kufanya udanganyifu huo watanyang’anywa leseni zao na kuwajibika kuwafidia wakulima wote walioathirika kutokana na matumizi ya pembejeo hizo bandia ambazo husababisha hasara katika uzalishaji wa mazao.

Serikali pia imewataka wakulima kuwa makini wanaponunua mbegu za ruzuku kwa kuhakikisha kuwa wananunua mbegu zilizofungwa kwenye kifungashio chenye lebo ya ubora ya TOSCI na wahakiki mbegu hizo kama ni halisi au feki kwa kukwangua kwenye lebo hiyo na kubonyeza kwenye simu zao *148*52#.

Pia, Naibu Waziri Silinde ametoa wito kwa wakulima kuendelea kujisajili katika mfumo wa ruzuku ya mbolea ili kuhakikisha udhibiti mzuri wa pembejeo za kilimo nchini.