Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MKOA WA DODOMA WATENGA EKARI 100 KWA AJILI YA KILIMOHAI

Imewekwa: 06 Mar, 2026
MKOA WA DODOMA WATENGA EKARI 100 KWA AJILI YA KILIMOHAI

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule ametoa ekari 100 kwa wadau wa Kilimo Ikolojia Hai kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo ikolojia hai hapa nchini na kuahidi Ofisi yake kuendelea kutoa ushirikiano.

Amesema hayo wakati wa hafla maalum ya ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Taasisi Mwamvuli ya Kilimo Hai Tanzania (TOAM) tarehe 5 Machi 2026, jijini Dodoma. Hafla hiyo ikiwa ni kilele cha Mkutano wa Nne wa wa Kitaifa wa Kilimo Ikolojia Hai (National Ecological Organic Agriculture Strategy - NEOAS) uliofanyika kuanzia tarehe 3-5 Machi 2026, katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.
 
Akitoa hotuba yake, Mhe. Senyamule amesema kuwa Mkoa wa Dodoma una ardhi nzuri na ya kutosha yenye rutuba inayoruhusu kilimo cha mazao aina mbalimbali.  
 
“Niwafahamishe kuwa Mkoa wa Dodoma huu wa sasa sio kama wa miaka mingi iliyopita ambapo tuliaminishwa kuwa ni nusu jangwa ila kwa sasa huu ni mkoa wa Kilimo tena ambao umeanza kuleta mapinduzi kwenye kilimo.  Kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, sasa wadau wa kilimo ikolojia hai nawasihi muendelee kufika Dodoma kuleta aina hii ya kilimo ambacho ndio kilimo kinachopendwa zaidi kwa sasa,” amesema Mhe. Senyamule.

Amebainisha kuwa Mkoa unashirikiana na Wizara ya kilimo katika kuwafikia wakulima huku akitolea mfano wa Kituo cha Umahiri katika Kilimo cha Bihawana kinachowapatia mafunzo wakulima kuhusu uhifadhi wa maji, matumizi bora ya mbolea, uandaaji wa udongo na huduma za ugani.
 
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter L.M. Msoffe amewataka wadau wa kilimo ikolojia hai kutambua kuwa Wizara ya Kilimo itaendelea kuunga mkono kazi zao kwa kuhakikisha elimu ya kilimo ikolojia hai inaendelea kutolewa katika Vyuo vya Kilimo vilivyopo nchini.
 
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa TOAM, Bw. Bakari Mongo mbali na kushukuru mchango wa Wizara ya Kilimo na Mkoa wa Dodoma katika kuendeleza kilimo ikolojia hai ametoa hamasa kwa wananchi kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na kilimo hicho na kueleza kuwa TOAM ipo tayari kutoa ushirikiano wakati wote.