MKOA WA PWANI WATENGA MAENEO YA KILIMO CHA MBOGAMBOGA
Serikali imetenga eneo la ekari 200 mkoani Pwani kwa ajili ya mradi mkubwa wa kilimo cha mazao ya matunda na mbogamboga, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya bustani na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo tarehe 16 Machi 2026, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) ameeleza kuwa eneo hilo liko katika kijiji cha Ruvu Station, kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.
Amesema mradi huo unalenga kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha Sekta ya Kilimo kupitia uzalishaji wenye tija na matumizi ya teknolojia za kisasa.
Katika hatua nyingine, Waziri Chongolo ameielekeza Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupeleka wataalamu wa kilimo cha matunda na mbogamboga mkoani Pwani ili kufanya tathmini ya udongo katika maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya kuanzisha mashamba makubwa ya kilimo hicho.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakari Kunenge amesema kuwa Mkoa wake umejipanga kutekeleza mradi huo na tayari umetenga maeneo matatu yanayofaa kwa ajili ya kilimo cha matunda na mbogamboga. Maeneo hayo ni Ruvu Station na Rupunga yaliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha; na Vikumvuru eneo lililopo wilayani Kisarawe.
Mhe. Kunenge ameeleza kuwa kuanzishwa kwa mashamba hayo kutachochea ukuaji wa uchumi wa wananchi na kuchangia kutimiza azma ya Mhe. Rais Dkt. Samia ya kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa chakula cha kujitosheleza na ziada yake kuilisha Dunia kibiashara.