MKUU WA MKOA KIGOMA AWATAKA WAKULIMA KUSHIRIKI KATIKA UPIMAJI WA AFYA YA UDONGO
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Sirro amewataka wakulima katika Wilaya, Kata na Tarafa za Mkoa huo kutoa ushirikiano kwa wataalamu wa Wizara ya Kilimo ambao wameanza upimaji wa afya ya udongo kwenye maeneo mbalimbali mkoani Kigoma.
Amesema hayo tarehe 12 Novemba 2025 wakati akizungumza na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo ambayo imeanza kupima afya ya udongo katika wilaya zote za mkoa huo, ikiwa ni mwendelezo wa shughuli ya upimaji wa afya ya udongo kwa nchi nzima inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo.
Mhe. Balozi Sirro amesema kuwa upimaji wa afya ya udongo ni kiungo muhimu katika kuendeleza Sekta ya Kilimo katika kujua uwezo wa kila eneo wa kuzalisha chakula.
"Wakati nikiwa Balozi nchini Zimbabwe nilishuhudia namna ambavyo wawekezaji kule wanathamini taarifa za afya ya udongo hivyo upimaji wa udongo kwao ni kitu muhimu kwa kuwa upimaji huo unawezesha kujua sifa na uwezo wa kila eneo katika kuzalisha mazao stahiki. Tanzania imeanza kupima afya ya udongo, hii ni wazi kuwa taarifa zitokanazo na upimaji huo zitasaidia kuinua kilimo. Niwasihi wakulima kushirikiana na wataalamu hawa ili mkoa unufaike,” amesema Mhe. Balozi Sirro.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo katika Wizara ya Kilimo, Mhandisi Godliver Mosha amebainisha kuwa zoezi la upimaji afya ya udongo litatekelezwa na timu ya wataalamu wasiopungua 40 kaa kushirikiana na Maafisa Kilimo katika Halmashauri za Mkoa wa Kigoma.
Aidha, tarehe 12 Novemba 2025 timu ya Wataalamu ikiongozwa na Injinia Mosha imetembelea Kata ya Kalinzi na Mkongoro na kuchukua sampuli ya udongo ambayo itapelekwa katika maabara kwa ajili ya kufanyiwa vipimo ambapo matokea yataelezea aina ya udongo uliopo, rutuba iliyopo katika udongo huo, aina na kiwango cha mbolea na mazao husika ya kulimwa.
Upimaji wa afya ya udongo umeshafanyika katika mikoa 10 na kutarajisa kumalizika Januari 2026 katika Mikoa iliyobakia nchini.