MRADI WA USTAHIMILIVU WAKE, DUNIA YETU (HROP) WAZINDULIWA

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), amezindua Mradi wa Ustahimilivu Wake, Dunia Yetu - Her resilience our Planet (HROP) tarehe 5 Juni 2025, jijini Dodoma.
Mhe. Silinde amesema kuwa Mradi huo unalenga kuimairisha utafiti wa mbegu bora za kilimo kwa kushirikana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), uwekezaji katika kilimo cha umwagiliaji, kuimairisha matumizi ya teknolojia zinazohimili mabadiliko ya tabianchi, vilevile Mradi huo utawezesha ushiriki wa vijana na wanawake katika kilimo.
Ameongeza kuwa Mradi utawawezesha wanawake kumiliki ardhi na kujihusisha na kilimo cha mashamba makubwa ya pamoja katika ngazi ya Halmashauri na amesisitiza kuwa Mradi uzingatie sera na miongozo kwa ajili ya kumkomboa mkulima, ambapo Wizara itaufuatilia Mradi huo kwa kila hatua ili kutekelezwa kwa yaliyokubaliwa.
Mradi huo unatekelezwa na Shirika la CARE International kwa kushirikiana na mashirika 6 (CARE Canada, WWF Tanzania, AGCOT, TGNP, Shahidi wa Maji na CFU-Tanzania. Mradi huo ni wa miaka 6 kuanzia mwaka 2024-2030, na unafadhiliwa na Serikali ya Canada kwa gharama zaidi ya shilingi Billioni 42 na unalenga kunufaisha zaidi ya wakulima 175,000.
Mradi huo utanufaisha vijiji 100 katika wilaya 5 ambazo ni Kilolo, Iringa, Mufindi, Wangingombe na Mbarali kwa Mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya.
Naibu Waziri Silinde amezindua Mradi huo kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb), ambapo washiriki wengine ni pamoja na Balozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Emily Burns, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Stephen Nindi, Mkurugenzi Mkazi wa CARE International Tanzania, Bi. Prudence Masako, Taasisi za Serikali pamoja na Washirika wa Maendeleo.