Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MWELI AKUTANA NA SPIKA WA BUNGE WA BELARUS

Imewekwa: 09 Jun, 2026
MWELI AKUTANA NA SPIKA WA BUNGE WA BELARUS

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amekutana kwa mazungumzo na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Belarus, Mhe. Natalya Kochanova tarehe 7 Juni 2026, ikiwa hitimisho la ziara ya kikazi nchini humo akimwakilisha Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo.

Wamejadili kuimarisha ushirikiano katika Sekta ya Kilimo kwa kuzishirikisha Sekta Binafsi kutoka nchi zote mbili kwenye biashara ya mazao, bidhaa mbalimbali za kilimo ikiwemo Kahawa, Chai, Korosho na mazao ya bustani (horticulture).

Aidha,  wamezungumza umuhimu wa watalaam kubadilishana uzoefu katika Sekta ya Kilimo, kuimarisha matumizi ya zana bora na za kisasa za kilimo yakiwemo matrekta  kama nyenzo muhimu ya kufanikisha mageuzi katika kilimo. 

Viongozi hao pia waneongea kuhusu fursa za uwekezaji katika tasnia ya mbolea kwenye ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mbolea kwa ajili ya matumizi ya Tanzania na nchi jirani zilizopo jirani katika jumuiya za SADC na EAC.

Katibu Mkuu Mweli ameeleza kuhusu Maonesho ya Kimataifa ya Wakulima ya Nane Nane 2026 ambapo ametoa mwaliko kwa Taasisi na Sekta Binafsi za Belarus kushiriki ili kuonesha bidhaa na teknolojia zao kwa wakulima wa Tanzania.

Viongozi hao wamekubaliana nchi hizo mbili kuendelea kutekeleza makubaliano ya ushirikiano katika Sekta ya Kilimo.