Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

MWELI: MILANGO YA WIZARA YA KILIMO IKO WAZI KUPOKEA MAONI NA USHAURI

Imewekwa: 26 Mar, 2026
MWELI:  MILANGO YA WIZARA YA KILIMO IKO WAZI KUPOKEA MAONI NA USHAURI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli ametoa wito kwa wadau wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi  kuwasilisha maoni, fursa au changamoto zozote  kwa kuwa milango ya Wizara hiyo iko wazi kuyapokea na kuyatatua ili kuzidi kuimarisha Sekta ya Kilimo nchini. 

Amesema hayo wakati wa Kikao cha Kikundi Kazi cha Tatu cha Kilimo cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), tarehe 25 Machi 2026, jijini Dodoma.

“Tunachokifanya hapa ni kuhakikisha Serikali inasikiliza mahitaji yenu kama wadau na kuweza kutatua kwa njia rahisi, hivyo nyie iweni huru kuja ofisini kwangu tujadiliane na kufikia muafaka namna bora ya kukuza Sekta hii ya Kilimo,” amesema Katibu Mkuu Mweli, ambaye ni Mwenyekiti wa kikundi hicho. 

Akitoa mchango wa maoni wakati wa kikao hicho, Katibu Mtendaji wa TNBC ambaye pia ni Katibu wa Kikao hicho, Dkt. Godwill Wanga, ameshauri Wizara ya Kilimo ifanye mapitio na kuona uwezekano wa kuondoa au kupunguza tozo na kodi katika Sekta ya Kilimo; kuongeza thamani katika mazao ili kuwezesha wakulima kukuza mitaji; kuongeza ajira na kuboresha maisha ya wakulima. 

Naye Mwenyekiti Mwenza wa Kikundi Kazi hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Bw. Virajlal Jituson pamoja na maoni mengine amekumbusha umuhimu wa kufanya utafiti wa kina kuhusu mienendo ya mabadiliko ya kisera ya Dunia, iwe athari za vita au mabadiliko ya tabianchi ili kuzidi kukuza Sekta ya Kilimo na uchumi kwa ujumla.

Kikao hicho kimejadili kwa upana na kufikia maazimio mbalimbali yakiwemo kuimarisha uzalishaji na utumiaji wa mbegu na miche bora kwa mazao na mifugo; kuboresha miundombinu na mifumo ya usafirishaji wa mazao na mifugo; kutunga sheria ya kulinda ardhi tengefu kwa ajili ya kilimo na mifugo; kuimarisha mfumo wa bei ya mazao; kuboresha mfumo wa uuzaji wa zana na bidhaa za kilimo; kurahisisha upatikanaji wa ajira na mikopo nafuu kwa vijana; kuvutia uwekezaji; na kuongeza uzalishaji wa mazao ili kupunguza utegemezi wa kuagiza kutoka nje ya nchi.