NAIBU WAZIRI SILINDE AKUTANA NA UJUMBE WA WABUNGE WASTAAFU WA CANADA KUJADILI FURSA ZA USHIRIKIANO SEKTA YA KILIMO
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), amekutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Chama cha Wabunge Wastaafu wa Canada (Canadian Association of Former Parliamentarians – CAFP), ukioongozwa na Bi. Yasmin Ratansi, tarehe 15 Aprili 2026, jijini Dodoma.
Lengo la mazungumzo hayo ni kujadili fursa za uwekezaji, kujifunza mazingira ya kilimo nchini Tanzania, pamoja na maeneo ya ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Canada.
Mhe. Silinde amesema moja ya maeneo muhimu ya kimkakati ni kupunguza uagizaji wa bidhaa za kilimo zenye uhitaji mkubwa kama vile ngano na mafuta ya kula, akieleza kuwa kwa sasa nchi inatumia kiasi kikubwa cha fedha za kigeni kuagiza bidhaa hizo.
“Tunaagiza ngano kutoka nje kwa gharama ya takribani Dola za Marekani Milioni 200 hadi 250 kwa mwaka. Vilevile, tunaagiza mafuta ya kula ambapo tunatumia takribani Dola za Marekani Milioni 250 hadi 300 kwa mwaka, pamoja na bidhaa nyingine mbalimbali za kilimo.” amesema Mhe. Silinde akieleza zaidi dhamira ya Serikali ya kutokomeza utegemezi wa kuagiza bidhaa hizo.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha kilimo cha umwagiliaji, kuongeza upatikanaji wa zana za kisasa za kilimo, pamoja na kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao kwa lengo la kuongeza ajira, hususan kwa vijana na wanawake.
Ameongeza kuwa Serikali inathamini ushirikiano na Serikali ya Canada na kubainisha kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo kupitia maeneo ya utafiti, miundombinu ya umwagiliaji, teknolojia za kilimo, na uwekezaji katika mnyororo wa thamani.
Naye Bi. Yasmin Ratansi ameeleza kuwa kuna mashirika kadhaa nchini Canada yenye nia ya kushirikiana na nchi za Afrika katika kukuza maendeleo endelevu, ikiwemo sekta ya kilimo. Amesema ziara hiyo imelenga kujifunza kwa undani kuhusu fursa zilizopo nchini Tanzania, changamoto zinazokabili sekta ya kilimo, pamoja na kubaini maeneo yanayoweza kuwekewa ushirikiano wa kiufundi na uwekezaji.
Ujumbe wa CAFP umeeleza dhamira ya kuendeleza mazungumzo na Serikali ya Tanzania kupitia njia rasmi za kidiplomasia na kushirikisha sekta binafsi ili kuharakisha matokeo chanya.