NIRC YAPONGEZWA KUIMARISHA USIMAMIZI WA MIKATABA YA MIRADI YA UMWAGILIAJI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli ameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa kuimarisha usimamiz wa miradi ya umwagiliaji, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani iringa ambapo amekagua pia Skimu ya Umwagiliaji Mkombozi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 56.
Katibu Mkuu Mweli pia amewataka Wahandisi wa Umwagiliaji nchini kuachana na kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kutumia mbinu bunifu na uzoefu wa kitaalamu katika kusimamia miradi ya umwagiliaji, ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija kwa Taifa.
Akifungua mafunzo ya usimamizi wa mikataba, sheria za ununuzi na utafiti wa miamba katika mabwawa mkoani Iringa, Bw. Mweli aliwataka wahandisi kufuta dhana ya kukariri kwa kuwa usimamizi wa wakandarasi unahitaji mbinu za ziada na kubadilishana uzoefu miongoni mwa wataalamu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wadau wengine.
“Utatuzi wa changamoto za miradi haujawahi kuandikwa wote kwenye makaratasi. Mara nyingine unakutana na mkandarasi mbishi, hapo ndipo unahitaji kuzungumza na mhandisi mwenzako aliyejua jinsi ya kumdhibiti. Msikae kama mnaogopana, kaeni pamoja mbadilishane mbinu za kiutendaji,” alisema Bw. Mweli.
Katibu Mkuu Mweli amebainisha kuwa mafunzo hayo, yanayofadhiliwa na Serikali kupitia Mradi wa TRIP 2 kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, yanalenga kuwajengea uwezo wahandisi kufanya maamuzi sahihi katika hatua za usanifu na ujenzi ili kupunguza athari na kuboresha ubora wa miradi.
Aidha, Mweli amewataka watumishi wa NIRC kuwa na uwezo mkubwa wa kuchambua taarifa za upembuzi yakinifu na kusimamia washauri waelekezi kwa umakini zaidi, ili miradi iwe na thamani ya fedha na kuleta matokeo makubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, ameshukuru ziara ya Katibu Mkuu Mweli huku akiwataka wahandisi wa mikoa kusimamia kwa nidhamu miradi mikubwa 146 inayotekelezwa na Tume, akisisitiza umuhimu wa uelewa wa sheria za ununuzi, usimamizi wa mikataba na makusanyo ya mapato ya ndani. Pia amehimiza wahandisi kushirikisha wananchi ili kuepusha migogoro yoyote.