PM MWIGULU: MKUTANO WA ACSAM 2026 UMEKUJA WAKATI MUAFAKA KWA MAGEUZI YA KILIMO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), amesema Mkutano wa Kwanza wa Afrika kuhusu Matumizi Endelevu ya Zana za Kilimo (Africa Conference on Sustainable Agricultural Mechanization - ACSAM) umefanyika kwa wakati muafaka kwa Tanzania kwa kuwa mageuzi ya kilimo yanahitaji zana jumuishi za kısasa na endelevu ili wakulima waweze kulima kwa tija zaidi.
Amesema hayo wakati akizindua Mkutano huo unaoanza tarehe 03 hadi 06 Februari 2026, katika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuni na mzizi wa tatizo kwenye masuala ya kilimo sasa vinaenda kupata suluhisho kupitia zana za kilimo. Hivyo, amewataka Washiriki kujadili na kutoka na malengo yatakayotekelezeka na kupimika ili Tanzania iwe na sekta ya kilimo ya kisasa, himilivu na yenye tija.
Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa changamoto zinazoikabili Sekta ya Kilimo ni pamoja na vijana kutojihusisha katika Kilimo kutokana na matumizi ya zana duni za kilimo; hivyo nguvu kazi katika kilimo kupunguza na kubaki kuwa ni wanawake jambo ambalo linasababisha uzalishaji usio na tija na kuleta tofauti za kijinsia katika kilimo.
Amesema mjadala kuhusu zana za kilimo kwa Kanda ya Afrika kupitia Mkutano huo ni ni suluhisho katika hii changamoto za vijana kutoshiriki katika kilimo na kusisitiza kuwa matumizi jumuishi ya zana za kilimo yataongeza ushiriki wa vijana katika kilimo. Hivyo, tija katika kilimo ajira na ustawi kwa vijana vitaongezeka.
Aidha, amewatakia washiriki wa Mkutano huo wa siku tatu mjadala mwema na kuwa Serikali itayafanyia kazi maazimio yatakayotokana na Mkutano huo.