PONGEZI WIZARA YA KILIMO KUFANYA KILIMO KUWA MGONGO KAMILI
Wizara ya Kilimo imepongezwa na Wakuu wa Mikoa nchini kwa kubadilisha falsafa ya kilimo ni uti wa mgongo kuwa mgongo kamili; na kuendelea kuwa daraja muhimu la mafanikio ya kilimo nchini.
Pongezi hizo zimetolewa wakati wa kikao kazi cha Wizara ya Kilimo na TAMISEMI kilichoshirikisha Wakuu wa Mikoa nchini tarehe 16 Aprili 2026, Hoteli ya St. Gasper, jijini Dodoma.
Kwa maoni tofauti, Wakuu wa Mikoa wameitaka Wizara ya Kilimo kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kuimarisha ushirika, kukuza majukwaa ya mazao kuwa ya kimkakati na mapinduzi kwa Sekta ya kilimo nchini. Wameongeza zaidi kuwa ushirikiano huu wa Wizara ya Kilimo na TAMISEMI ni ishara yenye dhamira ya kuboresha mazingira ya kiutendaji yanayogusia wakulima, moja kwa moja na kuleta matumaini na tija zaidi ya kipato kwa wakulima.
Akizungumza wakati wa kikao, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo amesema kuwa msukumo katika Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), chini ya uongozi wa Bi. Irene Mlola, Mkurugenzi Mkuu umewezesha COPRA kuwa chachu ya kuwezesha ujenzi wa Maabara Kuu ya Tafiti za Kilimo iliyopo Mtumba, mkoani Dodoma. Kadhalika, COPRA pia imewezesha ujenzi wa Maabara ya Kanda iliyopo Mkoani Morogoro kwa ajili ya tafiti za mbegu.
“Hongereni kwa kutengeneza mazingira yenye tija ya muda mrefu ya kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao ndani ya kanda saba inazozisimamia nchini na kilimo kuendelea kufanya vizuri kibiashara,” amesema Waziri Chongolo.
Kikao hicho pia kimewezesha Wakuu wa Mikoa kupata taarifa kuhusu Wakala ya Taifa ya Huduma za Ugani (NAESA) ambayo inatarakiwa kuanza mwezi Julai 2026.
Viongozi walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Mhe. Prof. Riziki Shemdoe (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI; Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo; Wakuu wa Mikoa nchini; wawakilishi wa menejimenti ya Wizara ya Kilimo na COPRA.