PROF. MSOFFE ASHIRIKI MKUTANO WA 34 FAO AFRIKA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Profesa Peter L. M. Msoffe, ameshiriki katika Mkutano wa 34 wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa Kanda ya Afrika, uliofanyika jijini Nouakchott, nchini Mauritania.
Katika mkutano huo, Prof. Msoffe amechangia mjadala kuhusu matokeo ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya FAO pamoja na vipaumbele vya Shirika hilo katika Kanda ya Afrika na kuhakikisha vipaumbele vinavyowekwa vinaendana na mipango na mwelekeo wa maendeleo wa nchi wanachama.
Aidha, amebainisha kuwa ni muhimu kuoanisha vipaumbele hivyo na sera na mikakati ya kitaifa, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 pamoja na Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Kilimo (AMP 2050), ili kufanikisha maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo.
Profesa Msoffe, ameambatana na Balozi wa Tanzania na Mwakilishi wa Kudumu katika Mashirika ya Kimataifa yaliyopo Roma, Italia, Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk; Katibu Mtendaji wa Baraza la Kumshauri Rais Masuala ya Chakula na Kilimo, Dkt. Florens Turuka; pamoja na wajumbe wa baraza hilo na wataalam mbalimbali.
Ushiriki huo umekuwa sehemu ya juhudi za Serikali kuimarisha mahusiano ya kimataifa, kutafuta rasilimali za kusaidia uwekezaji katika sekta ya chakula na kilimo, pamoja na kujifunza mbinu bora za kimataifa zilizochangia mageuzi ya sekta ya kilimo nchini.