Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

PROF. MSOFFE: USHIRIKIANO NA JICA KUIMARISHA KILIMO CHA KISASA

Imewekwa: 19 Feb, 2026
PROF. MSOFFE: USHIRIKIANO NA JICA KUIMARISHA KILIMO CHA KISASA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter L. M. Msoffe amesema kuwa Wizara itaendelea kusimamia kwa ufanisi miradi yote ya kilimo inayoendeshwa kwa ushirikiano na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) kuimarisha dhamira ya kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo nchini.

Prof. Msoffe amesema hayo tarehe 17 Februari 2026 mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la kubadilishana uzoefu wa shughuli zinazofanywa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan kupitia Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) na Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Amesema kuwa kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia, Tanzania imelekeza  juhudi za uendelezaji wa kilimo ambacho kitahitaji matumizi ya mashine za kisasa Ili kuongeza uzalishaji wenye tija.  “Yote hayo hayawezi kufanikiwa bila kutilia mkazi uendelezaji wa kilimo, na kilimo siyo kile kinachofahamika cha kutumia mkono, bali ni kilimo kitakachotumika kwa mashine za kisasa za kilimo,” amesema Prof. Msoffe.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA nchini, Bw. Ara Hitoshi amebainisha kuwa JICA imejipanga kuwafikia vijana wengi zaidi hapa nchini kwa kuwafundisha matumizi ya kisasa ya mashine za kilimo kama wanavyofanya vijana nchini Japan. 

Naye Naibu Makamu Mkuu wa SUA upande wa Utawala, Fedha na Mipango, Profesa Amandus Muhairwa amesema kuwa jukwaa hilolimekuwepo takribani miaka minne na limekuwa na manufaa kwa Tanzania kutokana na kutoa nafasi za kubadilishana uzoefu kuhusu masuala ya kilimo kinachoendana na mabadiliko ya tabianchi na teknolojia za kisasa.