RAIS NDAYISHIMIYE AMTAKA MWEKEZAJI ITRACOM KUWA BALOZI WA UWEKEZAJI TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Burundi, Mhe. Meja Jenerali (Mst) Evariste Ndayishimiye amemtaka mwekezaji wa kiwanda cha mbolea ITRACOM kuwa Balozi mzuri wa uwekezaji nchini Tanzania.
Rais Ndayishimiye amesema hayo wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha mbolea ITRACOM kilichozinduliwa jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 28 Juni 2025.
Rais Ndayishimiye ameeleza kuwa mwekezaji na mmiliki wa ITRACOM. Bw. Ntigacika Adrien anapaswa kuiwakilisha vema nchi ya Burundi katika masuala ya uwekezaji nchini Tanzania ili kuzidi kudumisha ushirikiano wa nchi hizo mbili hususan katika uwekezaji.
“Nampongeza sana Rais Samia kwa kukubali uwekezaji huu ufanyike Tanzania, hii imezidi kuimarisha ushirikiano wetu katika fursa za maendeleo,” amesema Rais Ndayishimiye.
Rais Ndayishimiye ameongeza kuwa uwepo wa kiwanda hicho cha ITRACOM utaongeza uzalishaji lakini pia usalama wa chakula utazidi kuimarika ikiwemo kuzidi kuchochea kilimo bora kwa wakulima.
Kiwanda cha ITRACOM Fertilizers Limited kina uwezo wa kuzalisha tani milioni moja (1,000,000) kwa mwaka kwa kutumia mitambo 5 ya kisasa inayozalisha tani laki mbili (200,000) kila moja kwa mwaka. Baadhi ya malighafi za samadi zinazozalishwa ni pamoja na mbolea asili kwa ajili ya kilimo hai, uchakataji wa mawe ya chokaa- kilimo, uchakataji wa madini ya fosifeti. Malighafi hizo huchanganywa na mbolea za kawaida za Urea, DAP na MOP ili kutengeneza mbolea za FOMI ambazo ni rafiki kwa udongo na mazingira.