RAIS SAMIA AMEWAHESHIMISHA WANA-BARIADI

“Mama umetuheshimisha wana-Bariadi. Hatukudai. Tunakupenda sana,” amesema hayo Mbunge wa Bariadi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrew Mathew akizungumza mbele ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa hadhara na wananchi wa Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu tarehe 18 Juni 2025.
Mhe. Rais Dkt. Samia amekuwa katika ziara Mkoani Simiyu ambapo amezindua miradi mbalimbali ya maendeleo vikiwemo viwanda vya kuchakata Pamba vya Moli Oil Mills Ltd. katika wilaya ya Bariadi; BioSustain Tanzania Limited katika Wilaya ya Meatu; na Shree Rajendra Agro Industry Limited kilichopo Wilaya ya Maswa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Kenani Kihongosi naye amepongeza hatua ya Wizara ya Kilimo kuweka Maafisa Ugani wa BBT ambao wamekuwa mkombozi kwa wakulima kwa kutoa elimu ya kilimo bora, matumizi sahihi ya mbegu na mbolea na kusimamia zoezi la upandaji kwa wakulima ambapo mavuno yameongezeka.
Ameeleza ziara hiyo imekuwa na mafanikio ambapo amezindua shughuli mbalimbali za maendeleo, hususan viwanda vya kuchambua Pamba.
“Tuendelee kulima kwa wingi, soko lipo na viwanda vipo ambapo leo nimezindua kiwanda cha Shree Rajendra Agro Industry Limited,” amesema Mhe. Rais Dkt. Samia.
Kiwanda hicho kimejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 12.4 ambacho kina uwezo wa kuchakata kilogram 350,000 za pamba mbegu sawa na tani 350 kwa siku.