RAIS SAMIA APONGEZWA KWA KUINUA TASNIA YA KOROSHO
Wadau wa Kilimo katika mnyororo wa thamani wa tasnia ya Korosho nchini wampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuinua zao hilo ambalo limekuwa likiendelea kufanya vizuri na kuleta tija kwa wakulima.
Wadau hao wamesema hayo wakati wa Kikao cha Tathmini ya Zao la Korosho kwa msimu wa 2025:2026, tarehe 14 Aprili 2026, ukumbi wa PSSSF Tower, jijini Dodoma.
Uzalishaji wa zao hilo umeongezeka kwa miaka mitatu mfululizo ndani ya uongozi wake Mhe. Rais Dkt. Samia kutoka tani 310,787 msimu wa 2023/2024 hadi tani 618,497 msimu wa 2025/2026; huku akisema kuwa ongezeko linatokana na ubanguaji kupitia mradi mkubwa wa kongani la viwanda vya kubangua korosho mkoani Mtwara na ongezeko kubwa la upandaji wa miche bora ya mikorosho ambapo katika msimu huu miche 4,220,000 imeshapandwa.
Akifungua Kikao cha Tathmini ya Zao la Korosho kwa msimu wa 2025:2026, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amesema kuwa dhamira ya Serikali katika zao hilo imelenga kuongeza uzalishaji wa Korosho ghafi hadi kufikia tani 1,000,000 na kuwezesha ubanguaji kwa asilimia 100 ifikapo mwaka 2029/2030.
Ameongeza kuwa ongezeko la uzalishaji katika zao la Korosho umewezesha Tanzania kuwa mwenyeji mtarajiwa wa Jukwaa la Dunia la Wadau wa Korosho (World Cashew Conference) linalotarajiwa kufanyika mapema mwaka 2027, Jijini Dar es Salaam.
Wadau hao pia wameishauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye tafiti za zao la Korosho ili kuongeza uzalishaji wa mbegu na miche inayokabiliana na mabadiliko ya tabianchi na visumbufu; kuongeza usambazaji wa pembejeo kwa wakati na mizani ya kidigitali, ikiwa ni pamoja na kuongeza huduma za ugani.
Viongozi mbalimbali wameshiriki wakiwemo Kamati ya Kusumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo; Waheshimiwa Mawaziri wa Sekta za Ujenzi; Uwekezaji; Wabunge; Wakuu wa Mikoa inayozalisha Korosho; Mhe. David Silinde (Mb), Naibu Waziri wa Kilimo; Bw. Gerald Mweli, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo; Brig. Jenerali (mstaafu) Aloyce D. Mwanjile, ndc
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania; Bw. Francis Alfred, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT).