Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

RAIS SAMIA AZINDUA KIWANDA CHA KISASA CHA KUCHAKATA PAMBA SIMIYU

Imewekwa: 18 Jun, 2025
RAIS SAMIA AZINDUA KIWANDA CHA KISASA CHA KUCHAKATA PAMBA SIMIYU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Kiwanda cha kisasa cha kuchakata Pamba kinachoitwa BioSustain Tanzania Limited katika Wilaya ya Meatu, Mkoani Simiyu tarehe 17 Juni 2025. 

Kiwanda hicho kina uwezo wa kuhifadhi tani 12,000 za Pamba ghafi na kuchakata kilo 500,000 sawa na tani 500 kwa siku kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Aidha, Dkt. Riyaz Haider, Mkurugenzi wa Kiwanda hicho amemueleza Mhe. Rais Dkt. Samia kuwa kinatoa uhakika wa soko kwa wakulima wa Pamba ambapo wananunua shilingi 1,200 kwa kilo ikiwa ni ongezeko la shilingi 50 ikilinganishwa na bei elekezi ya shilingi 1,150. 

Ameeleza kuwa ajira pia zimepatikana kwa Watumishi 1,205 ikiwa 375 ni ajira za kudumu na 830 ni ajira za msimu.  Dkt. Riyaz pia amesema kiwanda kimewezesha Maafisa Ugani 75 kwa kuwapatia pikipiki na mafuta Lita 5 kwa wiki ili kuwafikia Wakulima.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) ametoa rai kwa wanasiasa kutoingiza siasa kwenye zao la Pamba. Ameongeza kuwa Serikali inajenga mfumo mzuri kwa bei ya Pamba na hivyo Serikali iachiwe jukumu hilo la upangaji wa bei kulingana na Soko la Dunia.

“Bei ya Pamba itaendelea kuimarishwa karibia kila msimu kutoka ilipokuwa ikiuzwa kwa Shilingi 1150 kwa  kilogram na sasa bei ya kuanzia umefikia Shilingi 1,200 kwa kila kilo jambo ambalo limeendelea kuimarisha bei ya zao hilo,” amesema Waziri Bashe.