Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

RC BURIANI AHIMIZA UTAMBULISHWAJI MAENEO YA SHOROBA ZA KILIMO KANDA YA KASKAZINI

Imewekwa: 13 Feb, 2026
RC BURIANI AHIMIZA UTAMBULISHWAJI MAENEO YA SHOROBA ZA KILIMO KANDA YA KASKAZINI

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Batilda Buriani, amewataka Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga kubainisha na kuthibitisha maeneo yanayofaa kwa kilimo, ufugaji na uvuvi wenye tija katika ushoroba wa kaskazini.

Mhe. Buriani ametoa wito huo wakati akifungua Warsha ya Uhamasishaji na Uendelezaji wa Shoroba za Kilimo (AGCOT) kwa kanda ya kaskazini iliyoandaliwa na Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO) jijini Arusha, akisisitiza kuwa shoroba za kilimo ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Kilimo.

Amesema warsha hiyo imelenga kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa wataalamu wa mikoa na halmashauri kuhusu dhana ya shoroba za kilimo, nafasi yake katika kuchochea uzalishaji wa kibiashara, pamoja na wajibu wa wadau katika utekelezaji wake.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza kilimo cha kisasa chenye tija kwa kuzingatia mabadiliko ya tabianchi, akibainisha kuwa Sekta ya Kilimo imepangwa kama Sekta ya kuleta mageuzi katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kutokana na mchango wake mkubwa katika ajira, Pato la Taifa na fedha za kigeni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO), Bi. Elizabeth Missokia, amesema kuwa shoroba za kilimo ni maeneo ya kimkakati yanayounganisha uzalishaji, usindikaji, uchakataji, uhifadhi, usafirishaji na masoko kwa lengo la kuharakisha mageuzi ya kilimo chenye tija kuelekea uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050, kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa.