Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SEKTA BINAFSI KUSHIRIKISHWA PROGRAMU YA TFSRP

Imewekwa: 17 Sep, 2025
SEKTA BINAFSI KUSHIRIKISHWA PROGRAMU YA TFSRP

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inatambua na kuthamini mchango wa Sekta Binafsi katika mapinduzi ya kilimo kama ilivyoanishwa katika Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Sekta ya Kilimo (Agriculture Master Plan) akisema Serikali itaendelea kushirikiana nao katika nyanja mbalimbali za kisera, kiuchumi na uwekezaji.
 
Katibu Mkuu Mweli amesema hayo wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu cha tathmini kilichoandaliwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Benki ya Dunia tarehe 16 Septemba 2025, jijini Arusha ambacho kimelenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) katika kuboresha utekelezaji wake.
 
Ameainisha maeneo ya vipaumbele vya uwekezaji wa Sekta Binafsi katika mradi huu kuwa ni pamoja na uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa kilimo, ngano na mafuta ya kupikia, huku akiwataka kuangazia Ushirika ikiwa ni eneo rahisi katika usimamizi, akizitaka Sekta Binafsi kutembelea Vyama vya Ushirika na kujifunza katika kuwasaidia wakulima na kuishauri Serikali.
 
Kuhusu umuhimu wa mifumo ya TEHAMA, Katibu Mkuu Mweli amesisitiza inahitaji kusomana kwa kuwa tayari kuna mifumo kadhaa ya Serikali ambapo kupitia Programu ya TFSRP, mifumo iliyopo itaweza kutoa majibu na kujenga uwezo zaidi kwa watumiaji.
 
Katibu Mkuu Mweli pia ameongeza kuwa Wizara ya Kilimo (Bara) itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo (Zanzibar) katika kujifunza na kutekeleza Programu hii ambapo kwa hapa nchini imejikita katika vipaumbele vya utafiti, mbegu, huduma za ugani, afya ya udongo pamoja na upatikanaji wa bajeti kuu ya Sekta ya Kilimo.
 
Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula (TFSRP) inatekelezwa kwa miaka mitano (5) kuanzia mwaka 2023 hadi 2028 kwa zaidi ya Dola za Marekani milioni 300.

Kikao kimehusisha wataalamu kutoka Wizara za Kilimo (Bara na Zanzibar) na Taasisi zake; Taasisi Binafsi na Wadau wa Maendeleo (Benki ya Maendeleo ya Kilimo; na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan - JICA) na Wadau wengine muhimu katika mnyororo wa thamani wa kilimo.