Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SEKTA BINAFSI ZAHAMASISHWA KUWEKEZA KATIKA GHALA ZA KUHIFADHI MAZAO

Imewekwa: 19 Sep, 2025
SEKTA BINAFSI ZAHAMASISHWA KUWEKEZA KATIKA GHALA ZA KUHIFADHI MAZAO

Sekta Binafsi zimehamasishwa kujitokeza kuwekeza katika ghala zilizojengwa na Serikali katika maeneo mbalimbali nchini ili kuleta ufanisi na tija katika kukabiliana na changamoto ya upotevu wa mazao baada ya kuvuna (post-harvest lost) pamoja na kuimarisha usalama wa chakula nchini. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia Sehemu ya Usindikaji Mazao na Uongezaji wa Thamani katika Wizara ya Kilimo, Mha. Godwin Makori alipokua akiwasilisha utekelezaji wa vipaumbele chini ya Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula Tanzania (TFSRP), katika kikao kazi kilichofanyika tarehe 16 Septemba 2025, jijini Arusha kilicholenga kujadili na kutathmini utekelezaji wa Programu hiyo. 

Amesema Wizara ya Kilimo imelenga kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna hadi kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2030, malengo ambayo yatafikia   kupitia ujenzi wa miundombinu himilivu ya uhifadhi wa chakula, kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ili kuongeza ufanisi. 
 
Mha. Makori amesema katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Hati za Makubaliano 35 (MoU) zimesainiwa kati ya Wizara ya Kilimo, Halmashauri za Wilaya yalipojengwa maghala hayo kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha usimamizi, huku mikataba 36 ya uendeshaji maghala baina ya Wizara ya Kilimo, Halmashauri za vijiji na waendesha ghala binafsi na wa Umma ikisainiwa pia.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 Wizara imelenga kusaini Hati za Makubaliano (MoU) 44 na Mikataba ya uendeshaji ghala 44 kati ya Wizara, Halmashauri za vijiji na waendesha ghala, ambapo kati ya ghala hizo zaidi ya asilimia 50% watapewa waendesha ghala binafsi, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wa Sekta Binafsi katika eneo la usimamizi na uendeshaji wa ghala zilizojengwa na Serikali. 

Wizara kupitia programu ya TFSRP imesajili ghala za Umma na Binafsi 2330 na kukarabati zaidi ya ghala za Umma 28 kati ya 79 kwa lengo la kuweka mashine za kusafisha na kuchakata mazao katika ghala hizo.  Huduma hizo zitaendeshwa na Sekta Binafsi ili ziweze kutumika kwa ufanisi zaidi na kuongeza ubora wa mazao yanayohifadhiwa.