SEKTA YA KILIMO KUNUFAIKA NA MKUTANO WA TATU WA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI WA IRAN NA AFRIKA
Tanzania, kupitia Wizara ya Kilimo imeshiriki katika Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika (3rd Iran-Africa Cooperation Conference) tarehe 27 Aprili hadi 01 Mei 2025; unaoendana sambambana Maonesho ya Iran (Iranian Expo 2025), kuanzia tarehe 28 Aprili hadi 02 Mei 2025, katika mji wa Tehran.
Mkutano huo umefunguliwa na Rais wa Iran, Mhe. Masoud Pezeshkian tarehe 27 Aprili 2025 ambapo amesema kuwa Iran iko tayari kushirikiana na nchi za Afrika kwa kubadilishana mafanikio yake katika nyanja za Kilimo, Afya, Biashara, Viwanda, Usalama na Amani.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Hussein Mohamed Omar (anayesimamia masuala ya Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula) ameshiriki katika Mkutano huo muhimu; pamoja na Viongozi wengine kutoka zaidi ya nchi 50 za Bara la Afrika.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Omar amekutana kwa mazungumzo kwenye vikao vya pembezoni ya Mkutano huo na Viongozi na Wadau mbalimbali wakiwemo Naibu Waziri wa Kilimo wa Iran; Mamlaka ya Biashara ya Nje ya Iran; na Wafanyabiashara na Wazalishaji wa teknolojia mbalimbali.
Katika mazungumzo na Naibu Waziri wa Iran, nchi hiyo imeonesha nia ya kutaka kuwekeza nchini Tanzania katika Kilimo cha Ngano; huku Wafanyabiara mbalimbali wameonesha utayari wa kununua Chai, Kahawa, Korosho na Ufuta kutoka Tanzania.
Aidha, kuna Kampuni imeonesha nia ya kufanya biashara na Vyama vya Ushirika Tanzania kwa kubadilishana mashine za kuchakata ufuta kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile mafuta ya kula “edible oil”, n.k., kwa kubadilishana na ufuta badala ya fedha.
Kijiografia, Tanzania ipo katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo inakuwa na ushawishi wa kimkakati kwa nchi ya Iran katika kupanua wigo la soko kutokana na Tanzania kuwa lango la uchumi kwa mauzo na uagizaji / upitishaji wa bidhaa na nchi jirani. Hivyo, makampuni kadhaa ya Iran hayakusita kuonesha nia ya kushirikiana na Tanzania kwa mfano kupitia Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kwa kuleta mbolea aina ya UREA nchini na nchi za jirani.