SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA AFYA YA MIMEA KWA USALAMA WA CHAKULA NA LISHE NCHINI
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za afya ya mimea nchini kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) ili kuongeza tija katika Sekta ya Kilimo na kufikia malengo ya Agenda 10/30 na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Mhe. Silinde amesema hayo wakati akimwakilisha Mhe. Daniel Chongolo (Mb), Waziri wa Kilimo kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea yaliyofanyika katika Viwanja vya John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma tarehe 12 Mei 2026.
Aidha, Mhe. Silinde amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za kuimarisha huduma za kidijiti nchini, hatua ambayo imeendelea kuleta manufaa makubwa kwa wananchi. Pia amesisitiza umuhimu wa kuongeza jitihada katika kuimarisha ulinzi wa bayoanuai kwa ajili ya usalama wa chakula na lishe.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru, amesema kuwa Tanzania imefikia kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa asilimia 130 katika mwaka 2024/2025, huku uzalishaji wa chakula ukifikia tani 23,783,128. Ameeleza kuwa miongoni mwa mafanikio hayo ni udhibiti wa baa la panya uliofanyika katika mikoa 19 ambapo ekari 408,109 za mazao ziliokolewa na wakulima 66,511 kunufaika na hatua hiyo.
Mamlaka hiyo pia imefanikiwa kudhibiti zaidi ya ndege waharibifu milioni 231 aina ya kwelea kwelea waliovamia mashamba ya mpunga, mtama na uwele. Operesheni hiyo iliokoa takribani tani 1,611,000 za mazao. Katika kukabiliana na viwavijeshi, TPHPA ilifanya udhibiti katika hekta 219,411 kwenye wilaya 49 nchini na kuokoa zaidi ya tani 529,347 za mazao ya mahindi na mtama.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu : “Ulinzi wa Bayoanuai ya Mimea kwa Usalama wa Chakula na Lishe”.