Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SERIKALI KUENDELEZA PROGRAMU YA MIFUMO HIMILIVU YA CHAKULA

Imewekwa: 14 Oct, 2025
SERIKALI KUENDELEZA PROGRAMU YA MIFUMO HIMILIVU YA CHAKULA

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya amesema Wizara itaendelea na jitihada za makusudi katika kutekeleza Programu ya Mifumo Himilivu ya Chakula nchini (TFSRP) ili kukuza Sekta ya kilimo na kuleta maendeleo chanya kwa Taifa.

Amesema hayo tarehe 13 Oktoba, 2025 jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Mha. Kilindumya wakati wa kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Programu hiyo katika eneo la kupambana na tindikali udongo.  

Mha. Kilundumya amesema Programu itatoa dira kwa wadau katika tasnia ya mbolea kama vile kampuni za mbolea za ITRACOM, MINJINGU, Tanga Mine; pamoja na Kampuni ya Mbolea Tanzania ( TFC) ili kuona mbolea inayozalishwa inaleta matokeo gani  kwa jamii.

Aidha, Ofisi za kata, Maafisa Ugani pamoja na wasambazaji wa pembejeo (agro dealers) nao wanashirikishwa kwa ajili ya zoezi la usambazaji wa mbolea pamoja na tathmini ya matokeo kulingana na majukumu yaliyoratibiwa kwa kila mdau.

Majadiliano mengine kwenye kikao ni ushirikishwaji wa wadau katika utoaji elimu kwa wakulima, ukusanyaji wa taarifa za awali, upimaji wa tindikali (pH testing), ukusanyaji wa sampuli za udongo, matumizi ya bendera zenye jumbe rangi katika kubainisha kiwango cha tindikali katika eneo husika na utambuzi wa mashamba kidigitali.

Kikao hicho kimehusisha Wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC), ITRACOM, MINJINGU , Tanga Mine pamoja na Benki ya Dunia.