Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SERIKALI KUPUNGUZA GHARAMA ZA UZALISHAJI NA USAFIRISHAJI MAZAO SEKTA ZA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI

Imewekwa: 20 Feb, 2026
SERIKALI KUPUNGUZA GHARAMA ZA UZALISHAJI NA USAFIRISHAJI MAZAO SEKTA ZA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI

Serikali imelenga kuongeza uzalishaji na usafirishaji wa mazao katika Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuongeza thamani na kuvutia uwekezaji wa Sekta Binafsi katika kuongeza kipato cha wakulima, wafugaji na wavuvi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Uendelezaji na Ukuzaji wa Shoroba za Kilimo, Mifugo, na Uvuvi uliofanyika tarehe 20 Februari 2026, mkoani Mtwara, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Rajab amesema mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ina fursa kubwa za kimkakati katika utekelezaji wa shoroba za kilimo, mifugo na uvuvi kutokana na rasilimali ardhi na bahari pamoja na maziwa katika mikoa hiyo.

“Mikoa hii ina fursa kubwa za kimkakati katika utekelezaji wa shoroba za kilimo kutokana na rasilimali zilizopo, mazao ya kipaumbele ambayo ni korosho, ufuta, mbaazi pamoja na  choroko yanayozalishwa zaidi katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.  Vile vile, mazao ya mahindi, maharage, kahawa, soya na tumbaku yanazalishwa zaidi katika Mkoa wa Ruvuma,” amesema Mhe. Rajab.

Aidha, Mhe. Rajab ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo (ATO) na Shoroba za Kilimo Tanzania (AGCOT) inaendelea kuratibu utekelezaji wa miradi ya kimkakati nchini kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia za kisasa, huduma za Ugani, pembejeo za kilimo, ushiriki wa vijana na wanawake pamoja na kuzingatia mabadiliko ya tabianchi.

Pia amesema kuwa utekelezaji huo ni nyenzo ya kimkakati katika utekelezaji wa Agriculture Master Plan (AMP 2050) mpango huo umebuniwa ili kuunganisha maeneo yenye uzalishaji mkubwa na miundombinu muhumu ya barabara, reli, bandari, masoko, na viwanda pamoja na huduma za kifedha. 

Mhe. Zainab Rajab amesisitiza kuwa mkutano huo utawawezesha  wataalam kuelewa kwa kina dhana ya shoroba za kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na wajibu wao katika utekelezaji wake na namna ya kuzitafsiri Sera na Mipango ya Kitaifa kuwa ni miradi yenye matokeo chanya kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.