Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SERIKALI NA BENKI YA DUNIA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA MIKOPO YA KILIMO

Imewekwa: 20 Feb, 2026
SERIKALI NA BENKI YA DUNIA KUIMARISHA UPATIKANAJI WA MIKOPO YA KILIMO

Katibu  Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amekutana na Meneja kutoka Benki ya Dunia anayeshughulikia Chakula na Kilimo, Bi. Frauke Jongbluth tarehe 18 februari 2026 ofisini kwake- Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Katika mazungumzo yao, Katibu Mkuu Mweli amemweleza Bi. Frauke Jongbluth jinsi wakulima wanavyowezeshwa kunufaika na mikopo ya kilimo kwa riba nafuu huku pia wakipatiwa elimu ya kilimo kwa lengo la kuwawezesha kurejesha mikopo hiyo. 

Amebainisha kuwa wakulima kwa muda mrefu wamekuwa wakipata changamoto ya kukopeshwa kutokana na kuchukuliwa kama Sekta isiyo rasmi lakini kwa sasa mazingira ya wakulima kukopesheka yanazidi kuboreshwa, na kuwa Wizara itaendelea kuwaunganisha wakulima na wanunuzi wa bidhaa za mazao ili kuwawezesha kunufaika moja kwa moja na kilimo.

“Wizara inaendelea na jitihada za kuboresha kilimo hapa nchini kwa kuwakutanisha wakulima na masoko na kuwawezesha kupata mahitaji kama vile mbolea, huduma za ugani, matumizi ya teknolojia kwenye kilimo na kupewa huduma nyingine nyingi za kuwaendeleza,” amesema Bw. Mweli.

Kwa upande wake, Bi. Frauke Jongbluth amepongeza namna Wizara inavyoshughulikia kilimo na kuwa Tanzania ni kati ya nchi zinazotekeleza vema sera za kilimo ikiwa ni pamoja na usimamizi mzuri wa miradi ya maendelea ya kilimo.  Ameeleza kuwa Benki ya Dunia itaendeleza ushirikiano mzuri na Tanzania katika kuinua kilimo kwa kuwa kati ya nchi 13 inazozisimamia na inafanya vizuri.  Hivyo, Benki hiyo imeeleza ipo tayari kuendelea kukiwezesha kilimo cha Tanzania.