SERIKALI YAIMARISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ZA KISASA KUPITIA NDEGE NYUKI ZA KILIMO
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imezindua mafunzo ya siku kumi ya urushaji wa ndege nyuki za kilimo (agricultural drones) kwa wataalamu wa kilimo, ikiwa ni mkakati wa kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuongeza tija na kipato cha mkulima. Mafunzo hayo yameanza tarehe 29 Septemba 2025, jijini Dodoma.
Akifungua mafunzo hayo katika Viwanja vya Nane Nane vya John Malecela vilivyopo Nzuguni jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya, amewataka wataalamu wa kilimo kuhakikisha ujuzi watakaoupata unatekelezwa kwa vitendo na kuwanufaisha wakulima moja kwa moja.
"Tunapaswa kuhakikisha teknolojia hizi haziishii kwenye mafunzo pekee bali zinawafikia wakulima na kuleta matokeo chanya. Lengo la Serikali ni kumsaidia mkulima kuongeza kipato na kuifanya Sekta ya Kilimo kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi,” amesema Mha. Kilundumya.
Ameeleza kuwa ndege nyuki zikitumika kwenye shughuli za kilimo kama vile upimaji wa udongo, ufuatiliaji wa mashamba na matumizi ya viuatilifu zinakuwa zikichochea ufanisi na kupunguza gharama za uzalishaji.
Mafunzo haya yanaendeshwa na Kampuni ya ROKO DC kutoka India yakishirikisha wataalamu kutoka Idara na Taasisi mbalimbali za Wizara ya Kilimo na wadau wake wakiwemo Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Mamlaka ya Mbolea Tanzania (TFRA), Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) pamoja na Bodi ya Korosho.