SERIKALI YAPONGEZA MRADI WA VIJANA KILIMO BIASHARA, KUIBUA AJIRA NA MAGEUZI YA SEKTA KILIMO
Mradi wa Vijana Kilimo Biashara (VKB) wapongezwa kuwa chachu kwa vijana katika kuleta mageuzi kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo ikiwa pamoja na kuinua na kuimarisha vipaji vya vijana wajasirimali katika mikoa ya Dodoma na Singida.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Dkt. Stephen Nindi tarehe 30 Septemba 2025 Jijini Dodoma kabla ya kukabidhi zawadi kwa vijana wanufaika wa mradi huo na kuwapongeza Rikolto wanaotekeleza mradi kwa kuleta miradi yenye kuinua vijana kiuchumi kwenye shughuli za kilimo.
Mradi wa Vijana Kilimo Biashara (KVB) unafadhiliwa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na kutekelezwa katika Mikoa saba nchini (Singida, Dodoma, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Arusha na Manyara); ambapo katika mikoa ya Dodoma na Singida unatekelezwa na Rikolto katika Halmashauri 13 kwa bajeti ya shilingi bilioni 1.4 kwa mwaka.
Lengo kuu la mradi ni kuimarisha mfumo wa chakula kwa kuwawezesha vijana na wanawake kuongeza tija ya uzalishaji, kupata masoko, kuimarisha biashara zao na kuibua ajira mpya. Mradi huo unalenga kuwafikia vijana 40,000 wakiwemo wanufaika 36,000 sawa na asilimia 90 ya wanufaika wote, vijana wa kike wakiwa 25,000 sawa na asilimia 70 ya vijana wanufaika na wanaume 11,000 na watu wazima 4,000.
Katika kutekeleza mradi huo, Rikolto inatumia Program Atamizi (GFA), kama mbinu ya utekelezaji katika kuibua ubunifu kwa vijana wa kike na kiume wa umri wa miaka 18-35.
Vijana 423 walituma maombi ya kuonesha ubunifu wa kutatua changamoto zilizoko katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mtama, alizeti na mboga pamoja matunda; ambapo baada ya mchujo, vijana 100 walichaguliwa na pia vijana 94 walipata fursa ya kusaidiwa kuboresha biashara zao, kuongeza ujuzi na kuimarisha biashara kupitia kambi ya mafunzo.
Dkt. Nindi amesema ni matarajio ya Serikali kuona mradi huo unaleta tija na kuimarisha shughuli za kilimo biashara katika usindikaji, uhifadhi wa mazao baada ya mavuno, usafirishaji na usambazaji, ufumbuzi na utatuzi wa kidigiti, mifumo ya utunzaji wa taarifa na mbolea za asili.
Vijana 10 walioshinda watapata jumla ya Dola za Marekani 24,000 sawa na shilingi 59,317,440 kwa ajili ya kuendesha biashara ili kuongeza tija na ajira kwao na vijana wengine.