SERIKALI YATHIBITISHA KUWA NA AKIBA YA CHAKULA CHA KUTOSHA
Serikali imesema ina akiba ya chakula cha zaidi ya tani 555,000 inayotosheleza mahitaji ya nchi kwa kipindi cha zaidi ya miezi 21, iliyohifadhiwa katika maghala mbalimbali ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi yaChakula (NFRA).
Amesema hayo Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) wakati wa ziara ya ukaguzi katika ghala la kuhifadhia chakula lililopo katika Kanda ya Kipawa, Chang’ombe, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam tarehe 31 Januari 2026.
Ghala hilo linasimamiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) chini ya uongozi wa Afisa Mtendaji Mkuu, Dkt. Andrew Komba.
Waziri Chongolo amesema kuwa wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa chakula kutokana na akiba iliyopo inajitosheleza na ipo salama kwa matumizi. Ameeleza kuwa chakula kilichohifadhiwa kimezingatia vigezo vyote vya ubora na usalama vinavyotakiwa, hivyo kinafaa kwa matumizi ya binadamu.
Aidha, amewahimiza wakulima kuendelea kulima mazao ya muda mfupi ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuhakikisha uhakika wa masoko ya mazao yao.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA, Dkt. Andrew Komba amesema kuwa maghala ya NFRA yana chakula cha kutosha chenye ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa. Ameongeza kuwa chakula hicho hupitia ukaguzi na uhakikiwa mara kwa mara kutoka kwa taasisi zinazothibitisha ubora kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili kuhakikisha usalama na ubora wake kabla yakutumika.