SERIKALI YATOA MSISITIZO MARUFUKU UUZAJI WA MAZAO KWA “LUMBESA”
Serikali imepiga marufuku uuzaji wa mazao ya biashara kwa mfumo wa lumbesa na kusisitiza kuwa mazao yote yauzwe kwa kutumia vipimo sahihi vinavyotambuliwa kisheria. Pia watendaji wa Serikali watakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuwasaidia wananchi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Maelekezo yametolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) tarehe 10 Machi 2026, mjini Sumbawanga wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu katika Mkoa wa Rukwa.
Waziri Mkuu amewaagiza wanunuzi wote wa mazao kununua mazao kwa kufuata taratibu zilizowekwa na Serikali na kusisitiza umuhimu wa kuwalipa wakulima kwa wakati ili kulinda haki zao katika uzalishaji na uuzaji wa mazao yao. Utaratibu huo utasaidia kumkomboa mkulima kwa kuhakikisha anapata thamani halisi ya mazao yake kwa wakati.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inatekeleza skimu 18 za umwagiliaji zenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 ambazo zinafanyiwa upembuzi yakinifu kwa lengo la kuanza utekelezaji wake na kuongeza uzalishaji wa mazao katika eneo hilo.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu na mbolea bora ili kuongeza tija kwa wakulima, huku akisisitiza kuendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kuuza au kusambaza pembejeo feki ili kulinda wakulima dhidi ya hasara.