SERIKALI YAWAHAKIKISHIA HAKI ZAO WAFANYAKAZI 216 WA WATCO KULINDWA
Serikali imewahakikishia wafanyakazi 216 wa Kampuni ya Wakulima Tea Company (WATCO) inayomiliki viwanda vya Katumba na Mwakaleli wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, kuwa itasimamia kikamilifu na kuhakikisha hakuna haki yoyote ya mfanyakazi itakayopotea baada ya kusitishwa kwa mikataba yao ya ajira.
Wafanyakazi hao waliandamana hivi karibuni wakidai kulipwa fidia kutokana na kusitishiwa ajira zao bila kupata stahiki wanazostahili kisheria.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amezungumza na vyombo vya habari tarehe 9 Oktoba 2025 jijini Dodoma na kusema kuwa Wizara imefanya majadiliano ya wazi yaliyohusisha wawakilishi wa mmiliki wa viwanda hivyo, Bodi ya Chai Tanzania (TBT), Benki ya CRDB, pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi wa WATCO na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe.
Bw. Mweli amesema kikao hicho kimekubaliana kuhakikisha wafanyakazi wote wanapata haki na stahiki zao kwa mujibu wa sheria na kuongeza kuwa “changamoto iliyojitokeza ni kuwa wafanyakazi wamesitishiwa ajira bila kulipwa stahiki zao. Tumekubaliana kwamba hakuna haki ya mfanyakazi itakayopotea, na Wizara itaendelea kufuatilia kwa ukaribu hadi suala hili litakapomalizika.”
Kuhusu mustakabali wa soko la chai kwa wakulima wa Rungwe, Bw. Mweli alibainisha kuwa makubaliano yamefikiwa ili kuhakikisha kampuni ya WATCO, kupitia viwanda vyake vya Katumba na Mwakaleli, inaanza tena kununua majani ya chai na kuanza uzalishaji ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
“Niwahakikishie wakulima wote wa Wilaya ya Rungwe kuwa wataendelea kulima na kuuza majani ya chai katika viwanda hivyo kama awali. Benki ya CRDB ipo tayari kutoa fedha kwa mwekezaji wa sasa au mwingine yeyote atakayejitokeza kuhakikisha uzalishaji unaendelea,” ameongeza.
Aidha, amesema ndani ya miezi miwili ijayo, wafanyakazi waliokuwa wamesitishiwa mikataba watarejeshwa kazini mara tu shughuli za uzalishaji zitakapoanza upya.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Mweli ametoa siku saba kwa wamiliki wa WATCO kufika nchini ili kujadiliana Kwa kina kuhusu suala la mkopo wa kampuni hiyo na Benki ya CRDB, kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu.