Serikali yazibariki TARI, FAO na PHilMech kuunganisha nguvu kuwahudumia wakulima
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo Mha. Athumani Kilundumya amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko tayari kusimamia na kutoa ushirikiano kwa Taasisi za kilimo ili kuendeleza jitihada za pamoja kuwasaidia wakulima na kukuza sekta ya kilimo nchini.
Mha. Kilundumya amesema hayo leo Januari 30, 2026 jijini Dodoma alipotembelewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Shirika la kilimo na chakula Duniani (FAO) pamoja na Taasisi ya Ufilipino ya Maendeleo ya Teknolojia za baada ya Mavuno na Zana za Kilimo (PHilMech) ambao wameanza majadiliano ili kutekeleza shughuli za pamoja zinazolenga kuchangia kuinua sekta ya Kilimo.
Mha. Kilundumya amesema lengo la Tanzania ni kuzalisha kwa tija na hivyo kujitosheleza kwa chakula kama taifa pamoja na kulisha mataifa mengine.
Majadiliano ya Taasisi hizo yamejikita katika kuongeza matumizi ya zana za kisasa za kilimo pamoja na Teknolojia za baada ya mavuno lengo ikiwa ni kumrahisishia Mkulima kazi za shamba huku tija ikiongezeka.
Wakizungumza na Naibu katibu Mkuu, wahusika wa Taasisi zote wameonesha utayari wa kushirikiana ikiwa ni pamoja na kujengeana uwezo ili kumhudumia Mkulima hatua ambayo Mha. Kilundumya amesema watekeleze kwa haraka yale wanayokusudia kushirikiana ili kuchangia kuongeza tija katika sekta ya kilimo.