SILINDE ASISITIZA UMOJA NA UWAJIBIKAJI NIRC
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), amezindua Baraza la Sita la Wafanyakazi la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), huku akitoa wito kwa watumishi wa Tume kudumisha umoja na kutokubali kukatishwa tamaa na sauti chache za watu wasiothamini kazi nzuri inayofanywa na taasisi hiyo.
Amesisitiza kuwa uongozi ni dhamana ya muda na kila mtumishi ana wajibu wa kutimiza sehemu yake kwa uadilifu kabla ya muda wake kukamilika.
"Kuna watu wachache ambao kila siku wataongea vibaya, lakini msikubali sauti zao ziwafanye mfikiri jamii yote haitaki kazi yenu. Kila mmoja yupo hapa kwa sababu Mungu ana makusudi naye. Sisi sote tunapita tu, hakuna atakayekaa kwenye nafasi yake milele. Muhimu ni kufanya kazi kwa umoja kwa sababu kumkwamisha kiongozi mmoja ni kukwamisha maendeleo ya wananchi," amesema Mhe. Silinde.
Amesema mafanikio yanayoonekana ndani ya Tume hiyo yanatokana na uongozi imara, uwajibikaji wa watumishi pamoja na ushirikiano wa karibu uliopo kazini, jambo lililoongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yake hatua ambayo inaungwa mkono na
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na imai yake ya uwekezaji katika Kilimo cha Umwagiliaji.
“Kilimo ni Umwagiliaji Wizara inabebwa na umwagiliaji, Rais Dkt. Samia maagizo yake mengi ni kuhusu umwagiliaji hata hoja Bungeni za Wizara na Waziri Mkuu zinaelekezwa kwa asilimia 80 Umwagiliaji, hii imetokana na taasisi hii kuwa kubwa kwa sasa na kuwa kichochea katika kuongeza uzalishaji na kuwa na Kilimo biashara,”amesema Mhe. Silinde.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, amebainisha kuwa Tume imejipanga vizuri kwa mwaka wa fedha 2026/2027 katika kukamilisha, kuendeleza na kusimamia miradi iliyopo huku mkazo mkubwa ukiwekwa kwenye uboreshaji wa miradi na ulinzi wa ardhi kwa ajili ya wakulima wadogo.
Bw. Mndolwa amesema kumekuwa na changamoto baadhi ya watu wenye fedha kuanza kuwarubuni wananchi na kuwapora maeneo ya ardhi yenye miradi ya Umwagiliaji baada ya kuona Serikali imeweka miundombinu ya kisasa na maeneo hayo yanaenda kuwa na tija.
Aidha, mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mha. Saidi Ibrahim, amempongeza Mkurugenzi Mkuu na uongozi wake, akimtaja kama mlezi aliyefanikiwa kuimarisha mshikamano kati ya menejimenti na wafanyakazi.