SILINDE AZINDUA KITALU NYUMBA KUONGEZA MICHE BORA
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb), amezindua rasmi shamba la kitalu nyumba kwa ajili ya uzalishaji wa miche bora ya mbogamboga cha Raha Vegetable Farm, tarehe 18 Machi 2026 katika Kata ya Mkambarani, mkoani Morogoro, ikiwa ni juhudi za kuongeza wigo wa upatikanaji wa miche bora ya mbogamboga kwa wakulima hapa nchini.
Mhe. Silinde amesema kuwa kitalu nyumba hicho kinazalisha trei 16,000 kwa mwezi, na kuwa Raha Farm imeonesha mafanikio makubwa kwa kuhudumia wakulima kati ya 100,000 hadi 120,000 hapa nchini.
Amesisitiza kuwa Raha Vegetable Farm ni mfano wa vitendo, huku akihimiza wananchi kujikita zaidi katika uzalishaji wa miche na mbegu za kilimo, akibainisha kuwa ni fursa ya biashara yenye manufaa makubwa.
Aidha, Mhe. Silinde ameongeza kuwa Serikali imeweka kipaumbele katika kukuza sekta ya kilimo kupitia Ajenda 10/30, huku ikiendelea kuwawezesha vijana na wanawake kupitia programu ya BBT Mitaji. Kupitia mpango huo, wakulima wanapata mikopo nafuu kutoka Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF) kwa riba ya wastani wa asilimia 5 hadi 7, iwe kwa mtu mmoja mmoja au kwa vikundi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Raha Vegetable Farm, Bi. Raha Aloyce, amesema ataendelea kuzalisha miche bora ya mbogamboga na kujivunia kuajiri zaidi ya wafanyakazi 125. Amebainisha kuwa kampuni hiyo kwa sasa ina vitalu 13 katika mikoa ya Shinyanga eneo la Kahama, Dodoma eneo la Kibaigwa, Morogoro eneo la Dumila na Mkambarani, Tanga eneo la Kilindi kikunde na kuwa inawafikia wakulima popote walipo kupitia mfumo wa kidijitali.
Aidha, ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kumuwezesha kupitia mpango wa BBT Mitaji kwa mkopo wa Mfuko wa Udhamini wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), na kutoa wito kwa vijana na wanawake nchini kuchangamkia fursa hiyo ili kujikwamua kiuchumi kupitia sekta ya kilimo.