Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SILINDE: KILIMO IKOLOJIA HAI KUENDELEZWA

Imewekwa: 04 Mar, 2026
SILINDE:  KILIMO IKOLOJIA HAI KUENDELEZWA

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) ametoa rai kwa wakulima wanaojishughulisha na kilimo ikolojia hai kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kufikia malengo ya kilimo endelevu na kuwa na utoshelevu wa chakula kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira.

Naibu Waziri Silinde amesema hayo wakati akimwakilisha Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) kwenye Mkutano wa Nne wa wa Kitaifa wa Kilimo Ikolojia Hai (National Ecological Organic Agriculture Strategy - NEOAS), tarehe 3 Machi 2026, jijini Dodoma.

Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kufadhili utekelezaji wa mkatikati chini ya uratibu madhubuti wa kikosi kazi (National Implementation Task Force - ITF) ili kuleta mabadiliko makubwa katika Sekta ya Kilimo kwa lengo la kupunguza umaskini, kuongeza ajira hususan kwa vijana na wanawake na kufikia asilimia 10 ya ukuaji wa kilimo ifikapo mwaka 2030.

Ameongeza kuwa kaulimbiu “Kilimo Ikolojia Hai:  Kuimarisha Usalama wa Chakula na Lishe, Uhimilivu na Ustahimilivu wa Kiuchumi” inaenda sambamba na vipaumbele vya Wizara pamoja na mipango mbalimbali ya maendeleo ya kilimo ambapo Serikali imechukua hatua ya kuleta mapinduzi katika kilimo ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya kilimo kufikia trilioni 1.24 mwaka 2025/2026. 

Aidha, amewataka washiriki kujadili kwa kina namna ya kuendeleza jitihada mbalimbali za Kilimo Ikolojia Hai ikiwemo utekelezaji wa Mkakati wa Kilimo Ikolojia Hai 2023-2030; na Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Kilimo  2050 (Agriculture Master Plan 2050) ili kufikia malengo ya kilimo endelevu na kuwa na utoshelevu wa chakula kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira. 

Amesema kuwa Tanzania ina jumla ya mbegu za asili 770 za mazao ya ulezi, mpunga, mtama, uwele, migomba, maharage na papai ambapo kupitia TOSCI imekamilisha utambuzi wa aina 13 za mbegu za asili za mahindi, mpunga, maharage na papai ambazo zimeingizwa kwenye mfumo rasmi wa mbegu huku TARI inaendelea kukusanya, kusafisha na kutunza aina 360 ya mbegu za asili za mazao ya mpunga, ufuta, uwele, ulezi, choroko, kunde, migomba, korosho, viazi vitamu, pilipili manga, tango, mbaazi na soya.