SILINDE: WAKULIMA LIMENI TENDE INASTAHIMILI UKAME
Wakulima wamehimizwa kulima zao la Tende kutokana na uwezo wake wa kustahimili ukame na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, sambamba na kuongeza kipato na ustawi wa maisha yao.
Ametoa wito huo Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa na rasilimali za kuendeleza zao hilo chini ya mradi wa “Emergency and Resilience Building Support for Smallholder Farmers Affected by Drought through Exploratory Date Palm Cultivation in Tanzania,” tarehe 15 Septemba 2026, katika Maabara Kuu ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), jijini Dodoma.
Ameishukuru Serikali ya Ufalme wa Saudi Arabia kupitia KSRelief kwa ufadhili wa mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani 978,000 ambapo KSRelief imeratibu na kutoa msaada wa kitaalamu kwa kushirikiana na TARI katika kufanya utafiti na kutekeleza shughuli za mradi.
“Wizara ya Kilimo itaendelea kuhakikisha vifaa na rasilimali zilizokabidhiwa, ikiwemo trekta, mifumo ya umwagiliaji na vifaa vya maabara, vinatumika kikamilifu ili wakulima wengi zaidi wapate miche ya Tende na mafunzo ya kustawisha zao hilo nchini,” amesema Naibu Waziri Silinde.
Kwa upande wake, Balozi wa Ufalme wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Mhe. Yahya Okeish amesema kuwa mradi huo unaimarisha zaidi ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya kilimo, usalama wa chakula na maendeleo ya jamii.
Mradi huo pia umehusisha Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambapo Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania, Dkt. Nyabenyi Tipo, amesema kuwa FAO imechangia Dola za Marekani 234,000 katika mradi huo (Technical Cooperation Programme). Ameongeza kuwa mradi huo unalenga kuleta uzoefu wa kilimo cha Tende kutoka Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini na kuutumia katika mazingira ya Tanzania ili kuongeza ustahimilivu wa wakulima dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza kuhusu utafiti wa zao hilo, Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, amesema kuwa utafiti umeonesha kuwa udongo wa Dodoma unafaa kwa kilimo cha Tende ambapo tayari miche 3,700 ya awali imeanza kusambazwa kwa wakulima. Amebainisha kuwa TARI itaendelea kuzalisha miche mingine kupitia mradi huo ili wakulima wasambaziwe miche ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha Tende.