Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TANZANIA, BENKI YA DUNIA KUIMARISHA USHIRIKIANO KILIMO

Imewekwa: 13 May, 2026
TANZANIA, BENKI YA DUNIA KUIMARISHA USHIRIKIANO KILIMO

Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde (Mb) amekutana kwa mazungumzo na Bi. Anna Wellenstein, Mkurugenzi wa Kanda wa Benki ya Dunia anayeshughulikia masuala ya Mazingira (Planet) katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, tarehe 11 Mei 2026 jijini Dodoma.

Viongozi hao wamejadili maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa Programu ya Mifumo Himilivu ya Usalama wa Chakula Tanzania (TFSRP), Mpango wa AgriConnect Compact Agreement pamoja na kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Serikali na Taasisi hiyo ya Kimataifa.

Naibu Waziri Silinde amebainisha kuwa ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia wa zaidi ya miongo mitano umekuwa nguzo muhimu katika mageuzi ya Sekta ya Kilimo nchini ambapo matokeo chanya yanayoonekana. Hii ni pamoja na ugunduzi wa aina mpya za mbegu zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi, utoaji wa mafunzo kwa maafisa ugani, kilimo cha umwagiliaji na uimarishaji wa afya ya udongo.

Amesema kuwa ,Wizara ya Kilimo  itahahakikisha utekelezaji wa Mpango wa AgriConnect unafanikiwa kwa manufaa ya wakulima nchini. Mpango huo mpya wa kimkakati unaoshirikisha Benki ya Dunia una lengo la kuchochea uwekezaji wa Sekta Binafsi na kukuza biashara ya kilimo katika minyororo ya thamani ili kuongeza tija na kipato kwa wakulima.

Kwa upande wake, Bi. Anna Wellenstein amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya kilimo nchini inayofadhiliwa na Benki ya Dunia na amepongeza jitihada za Serikali katika kuhakikisha usalama wa chakula.  Amesisitiza kuwa Benki ya Dunia itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa Tanzania katika kuhakikisha Sekta ya Kilimo inafikia malengo iliyojiwekea ikiwepo kuimarisha usalama wa chakula na kuongea tija na kipato kwa wakulima.