Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

TANZANIA, INDONESIA KUIMARISHA MAFUNZO YA WAKULIMA MKINDO

Imewekwa: 07 May, 2026
TANZANIA, INDONESIA KUIMARISHA MAFUNZO YA WAKULIMA MKINDO

Ujumbe kutoka Wizara ya Kilimo ya Jamhuri ya Indonesia umepokelewa na Wizara ya Kilimo nchini na kufanya ziara ya ukaguzi katika kituo cha mafunzo kwa wakulima cha Mkindo, Mkoani Morogoro tarehe 6 Mei 2026.

Ziara hiyo ni sehemu ya Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano katika Sekta ya Kilimo baina ya Tanzania na Indonesia (4th Joint Agriculture Cooperation Commitee-JACC), kwa dhumuni la kutembelea kituo hicho kinachoendeshwa kupitia ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Indonesia.

Serikali ya Jamhuri ya Indonesia imetoa msaada wa Dola za Marekani 547,624 katika ujenzi wa darasa 1 lenye uwezo wa kutumiwa na  wanafunzi 80; ujenzi wa bweni 1  pamoja na ukarabati wa bweni 1 ambapo baada ya kukamilika litawezesha kituo hicho kuwa na uwezo wa kupokea wakulima 64 ndani ya bweni.

Fedha hizo pia zitawezesha ukarabati wa vyoo; ununuzi wa gari, pikipiki, powertiller, planter,  kompyuta, talakilishi, vitanda na magodoro pamoja na printer,  ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa visima na ujenzi wa uzio kuzunguka chuo.

Wakati wa ziara na majadiliano yaliyofanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Wakulima cha Mkindo, Mhe. Priadji Soelaiman, Naibu Balozi wa Indonesia na Mkuu wa Masuala ya Uchumi nchini Tanzania, kwa niaba ya Serikali ya Indonesia, ametoa shukrani kwa Wizara ya Kilimo ya Tanzania kwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa katika utekelezaji wa mradi huo na kueleza Serikali yake itaendelea kutoa ushirikiano katika hatua za utekelezaji zilizosalia na maeneo mengine kama vile tafiti, maauala ya masoko na zana za kilimo.

Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mafunzo na Utafiti kutoka Wizara ya Kilimo, Bw. Godfrey Edward amesema kuwa ushirikiano huo unaendelea  kuwajengea wakulima uwezo kupitia mafunzo ya vitendo na matumizi ya teknolojia bora za kilimo nchini. 

Kituo hicho kimeanza rasmi kutoa mafunzo kwa wakulima mnamo mwaka 1996 na kunufaisha jumla ya wakulima 9654 pamoja na maafisa ugani 1783 nchini, kikilenga kutoa elimu zaidi katika mazao ya mpunga ,kakao, vanilla, chikichi, hotikacha pamoja na tufaha.