Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Wizara ya Kilimo

SEKTA YA KILIMO KUNUFAIKA NA MKUTANO WA NGUVU ZA ATOMIKI

Imewekwa: 17 Sep, 2025
SEKTA YA KILIMO KUNUFAIKA NA MKUTANO WA NGUVU ZA ATOMIKI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mhandisi Athuman Kilundumya anashiriki katika Mkutano Mkuu wa 69 wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki unaoendelea Jijini Vienna, nchini Austria kuanzia tarehe 15-19 Septemba 2025.

Ushiriki wa Wizara ya Kilimo katika Mkutano huo ni muhimu ikizingatiwa kuwa Wizara imeanzisha Mpango wa ATOMS4FOOD kupitia Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani. Mpango huo utasaidia Tanzania katika utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Kilimo "Agricultural Master Plan 2050 “ pamoja na Agenda 10/30 ambapo vyote kimsingi vimelenga kuleta mageuzi makubwa kwenye Sekta ya Kilimo ikiwemo kuongeza uzalishaji wenye tija, kuimarisha usalama wa chakula na kufungua masoko ya mazao ya kilimo.

Mpango wa Atoms4Food unalenga kutumia teknolojia ya mionzi katika uzalishaji wa mbegu bora zinazohimili mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi mazao ya chakula, kuboresha afya ya mimea na udongo.

Ujumbe kutoka Tanzania katika Mkutano huo unaongozwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Ignatius Nombo ambapo pia Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Usalama wa Chakula kutoka Idara ya Masoko na Usalama wa Chakula, Bw. Aradius Kategano anashiriki.