TANZANIA MSHINDI WA KWANZA UTEKELEZAJI WENYE UFANISI, MIRADI INAYOFADHILIWA NA GAFSP
Tanzania imekuwa ya kwanza Barani Afrika kutokana na utekelezaji wenye ufanisi katika Miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Kusaidia Programu za Kilimo na Usalama wa Chakula (GAFSP), ikiwa ni kati ya miradi 13 inayotekelezwa na Shirika hilo, ambapo kwa hapa nchini Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC) unaotekelezwa na Wizara ya Kilimo umeshinda tuzo hiyo kwa mwaka 2025.
Tuzo hiyo imepokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli tarehe 01 Septemba 2025 jijini Dodoma, ambapo ametoa pongezi kwa watendaji wa Mradi wa TANIPAC kwa utendaji mzuri uliofanikisha Tanzania kupata tuzo hii.
Ushindi huu ni matokeo ya Mradi huu kukidhi vigezo kama kuleta matokeo yaliyokusudiwa, kutoa taarifa za mradi kwa muda unaohitajika, na matumizi mazuri ya fedha ambapo hadi kufikia sasa mradi umetumia takribani 99% ya fedha.
Mradi wa TANIPAC unatekelezwa kwa shilingi bilioni 80 kwa ubia kati ya Serikali, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), na Mfuko wa Dunia wa Kusaidia Programu za Kilimo na Usalama wa Chakula (GAFSP). Mradi unatekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama maghala katika halmashauri 12 za Tanzania Bara na Zanzibar, kituo cha mazao baada ya kuvuna kilichopo Mtanana, Wilaya ya Kongwa, maabara ya kibaolojia iliyopo. Wilayani Kibaha na Maabara Kuu ya Kilimo iliyopo Mtumba jijini Dodoma.
Aidha, mradi umetoa elimu ya kudhibiti sumukuvu katika mnyororo wa thamani wa mazao kwa wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wasafirishaji na wasindikaji.